• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
UMBEA: Dalili mnaishi kama wapangaji wawili wala sio mtu na mwenzake

UMBEA: Dalili mnaishi kama wapangaji wawili wala sio mtu na mwenzake

Na SIZARINA HAMISI

KUNA dalili ambazo kama zinatawala uhusiano wako kwa muda mrefu, huenda ndoa ama uhusiano wenu upo njiani kusambaratika.

Viashiria hivi vinapoanza kuonekana bayana, basi ni muhimu kuangalia jinsi ya kuepusha kuvunjika kwa ndoa ama uhusiano, iwapo bado unayo nia hiyo.

Dalili hizo ni pamoja na;

• Kuwa na hasira zisizoisha, hasa unapomuona mwenzako

Pale unapoona kila wakati unapomuona mwenzako, hasira zinatawala nafsi yako ama unakuwa na hamaki isiyoisha, unapaswa kujua kuwa mambo yamebadilika.

Ukiona hivyo ujue kabisa ni kwa sababu penzi lenu limeanza kupungua au kuisha hivyo unakosa uvumilivu. Katika hali kama hii, mwenzako anaweza kuropoka hata akiwa katikati ya watu na wala hatajali unavyojisikia kwa yeye kufanya hivyo. Utashangaa na kujiuliza mbona huko mwanzoni aliweza kunivumilia? Jibu ni kwamba penzi limepoa au kuisha.

• Unakosa furaha unapokuwa naye

Kwa kawaida mwanaume anavyompenda mwanamke huwa na kiu ya kumfurahisha. Hufanya vitu kuhakikisha mpenzi wake anatabasamu na anajisikia murua. Kila siku kiu ya mwanaume ni kuona mwanamke huyo anatamani kuendelea kuwa ndani ya penzi hilo. Mapenzi yakiisha vitu hivi vyote vinayoyoma na kupeperukia mbali.

• Unakosa muda wa kuwa na mwenzako

Ishara nyingine ya mapenzi ya mwanaume yanapokwisha kwa mpenzi wake ni kukosa kabisa kuwa na muda naye.

Mwanzoni mlikuwa mnakuwa na muda wa pamoja, sasa hapati tena muda huo na kila ukiuliza unapewa visingizio. Mara kazi, mara nimechoka, mara safari, mara ninaugua. Yaani inakuwa ni bora autumie muda wake akiwa na marafiki zake kuliko kuwa na wewe. Vile vicheko vya pamoja mkiwa peke yenu vyote vinakwisha. Ukiona hivyo, ujue hapo kuna walakini.

• Hakujali tena

Kawaida mwanaume anapoacha kumpenda mwanamke huwa anapunguza au kuacha kumjali na kumhudumia mpenzi wake. Inakuwa ni vigumu kwake kukuhudumia. Atawatendea wengine mema na kuwajali, lakini sio wewe. Zile bashasha na mapenzi aliyowahi kuwa nayo hutoweka.

• Kuvunjika mawasiliano

Mapenzi ya mwanaume yanapopungua au kuisha kwako utaona jinsi inavyokuwa vigumu kwake kuwasiliana nawe. Unapomwonyesha umuhimu au uhitaji wako wa mawasiliano yeye anaona ni mzigo mkubwa. Anakuwa mzito kuzungumza, mgumu kuonyesha hisia zake kwako, mara nyingine inakuwia vigumu kugundua lini amefurahi na lini amekasirika. Unabaki unajiuliza, hapo awali alikusikiliza, siku hizi hakusikilizi tena. Zamani ulijua alipo na anachofanya siku hizi ukiuliza unazua ugomvi. Ukiona hivi, ni dalili kuwa penzi lake kwako linayoyoma.

• Siri zinakuwa nyingi

Mwanaume anapompenda mwanamke humruhusu mwanamke huyo kuyajua maisha yake. Maisha ya mwanaume huyu yanakuwa kama kitabu kilicho wazi. Hafichi kitu wala kuishi maisha ya kona kona. Tofauti yake ni kwamba mapenzi yakimwisha utaona siri zinaanza kuwa nyingi, haujui nini kinaendelea kwenye maisha yake na wala haoni umuhimu wa kukushirikisha kwa kinachomhusu yeye. Utamuona katoka, karudi, kaingia huku na kutoka kule bila kukueleza kinachoendelea.

• Ushirikiano unatoweka

Penzi la mwanaume linapoisha juu yako mara nyingi huwa anaona shida kukushirikisha kwenye maisha yake au yeye kushiriki maisha yako. Furaha yake inakuwa yake na yako inabaki kuwa yako wakati mwanzoni furaha yako ilikuwa furaha yake. Ukifanikiwa, naye anajisikia furaha, lakini siyo sasa.

Inapofikia hatua hii, ndipo pale mnapoishi nyumba moja kama wapangaji wawili na sio mtu na mwenzake.

Ukiona mambo haya yanatokea, utambue kwamba, hizi ni siku za mwisho za penzi lenu.

 

[email protected]

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Sili silali baada ya mpenzi kukataa...

SHERIA: Sheria haitambui tamaduni za kurithi wajane

adminleo