Makala

SHERIA: Sheria haitambui tamaduni za kurithi wajane

August 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

BAADHI ya jamii za humu nchini huwa zinaendeleza utamaduni wa kurithi wajane kama ilivyodhihirika wazee walipomtaka mjane wa aliyekuwa mbunge wa Kibra Ken Okoth aende kijijini kurithiwa.

Hata hivyo, kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, mjane hawezi kulazimishwa kurithiwa na ndugu ya marehemu mumewe. Kwa ufupi ni kuwa, japo sheria inatambua ndoa za kitamaduni, haitambui desturi zinazoenda kinyume na sheria.

Desturi ya kitamaduni ambayo sheria ya ndoa inatambua kwa uwazi ni mfumo wa ulipaji mahari wa jamii tofauti za Kenya. Kuhusu wajane sheria inasema wanaweza kuamua kuolewa tena. Hapa inamaanisha ni lazima sheria ifuatwe kikamilifu.

Kwa vile sheria inasema ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanamume na mwanamke, kulazimisha mjane kuolewa na ndugu au jamaa wa familia au ukoo ni kinyume cha sheria.

Hivyo basi, jamii au familia haifai kumlazimisha mjane kurithiwa isipokuwa yeye binafsi aamue kuolewa na ndugu au mtu wa familia ya marehemu mumewe.

Ni muhimu kuelewa kuwa baadhi ya tamaduni zinaenda kinyume cha sheria kwa sababu ni makosa watu wenye uhusiano wa damu au familia kuoana.

Ni suala linalohitaji tafsiri ya kindani kwa sababu mwanamke akiolewa huwa sehemu ya familia ya mumewe.

Kulazimu

Wajane wanapaswa kufanya uamuzi wao binafsi kuhusu jinsi wanavyotaka kuishi.

Hawafai kulazimishwa kurithiwa na jamaa za marehemu.

Wanaowalazimisha huwa wanavunja sheria ya ndoa ya Kenya.

Aidha, desturi za ndoa za kitamaduni zinaweza kufuatwa iwapo ndoa ilikuwa ya kitamaduni na sio kwa ndoa za kijamii au za Kikristo.

La muhimu na kimsingi ni kuwa mwisho wa ndoa ni kifo na wajane wana uhuru wa kuamua wanavyotaka kuishi baada ya waume zao kuaga dunia.

Kurithi wajane hakuna msingi wa kisheria na ni kuwahangaisha bure. Ni makosa kuamini mke huwa wa jamii.