Sukari yenye sumu yatoweka kimiujiza kutoka stoo Pwani
Na MOHAMED AHMED
JUHUDI za serikali kuwalinda Wakenya dhidi ya sukari inayoaminika kuwa na sumu zimegonga mwamba baada ya magunia 5,000 ya sukari hiyo kusambazwa sokoni ghafla.
Magunia hayo yaliibwa na kutoweka katika muda wa wiki tatu kutoka kwa bohari la Bollore, lililoko Changamwe, Mombasa.
Wadokezi wa Taifa Jumapili wanasema kuwa baadhi ya sukari hiyo imeanza kuuzwa jijini humo.
Polisi wanasema magunia mengine 300 ya sukari ambayo ni nzuri kutumika pia yaliibwa kutoka kwa bohari hilo.
Kamanda wa polisi eneo la Changanwe, Bw Daudi Loronyokwe alisema mlinzi wa bohari hilo ametoroka na tayari anasakwa.
“Tayari tunamsaka mlinzi ambaye alitoroka muda tu baada ya ripoti ya wizi huo kufikishwa kwa polisi,” akasema Bw Loronyokwe.
Kulingana na ripoti za polisi, gari moja lilionekana katika bohari hilo likijaribu kupakia magunia hayo ya sukari.
Gari hilo lilionekana na msimamizi wa walinzi wa bohari hilo alipokuwa anapiga doria yake ya kawaida.
“Msimamizi alikuwa anaangalia wenzake waliokuwa kazini ndipo alipoona gari hilo. Alipoliamuru kusimama liliweza kutoweka,” akasema Bw Loronyokwe.
Alisema kuwa baada ya polisi kufika eneo hilo walikuta kufuli la bohari hilo limeregeshwa kana kwamba hakukuwa na kitu kimefanyika.
“Baadhi ya magunia hayo yalionekana yametapakaa eneo hilo na hivyo basi tunaamini kuwa wizi huu umehusisha watu wa ndani,” akasema kamanda huyo wa polisi.
Washukiwa saba wakamatwa
Jumamosi, Bw Loronyokwe alisema washukiwa saba wamekamatwa kuhusiana na wizi huo.
Aidha, alisema mmiliki wa sukari hiyo nyingine yupo Nairobi.
Kuhusiana na sukari hiyo mbaya, Bw Loronyokwe alisema imekuwa katika bohari hilo kwanzia mwaka jana ambapo serikali ilianzisha operesheni dhidi ya sukari mbovu.
Baada ya operesheni hiyo, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alisema sukari hiyo ilikuwa na sumu aina ya ‘mercury’.
Kulingana na upekuzi uliofanywa dhidi ya magunia 1,400 kati ya yale yalionaswa katika maeneo tofauti ya nchi, iligundulika kuwa sukari hiyo ipo na sumu hiyo.
Baada ya operesheni hiyo, sukari hiyo imesalia katika mabohari tofauti nchini huku serikali ikilaumiwa kwa kutoiharibu mapema.