Starlets kumenyana na Zambia mechi ya kirafiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, itafunga safari ya kuelekea jijini Lusaka mnamo Alhamisi kupimana nguvu dhidi ya wenyeji Zambia.

Starlets ya kocha Richard Kanyi, ambayo siku chache zilizopita ilikaribisha kocha wake wa zamani David Ouma, italimana na She-polopolo mnamo Machi 25 uwanjani Arthur Davies mjini Kitwe unaopatikana kilomita 358 kutoka Lusaka, kaskazini mwa Zambia.

Washindi wa medali ya fedha ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mwaka 2016, Kenya, wamekuwa wakijinoa uwanjani Kenyatta mjini Machakos. Wanajiandaa kulimana na Uganda mara mbili katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2018.

Starlets itakabana koo na Uganda mnamo Aprili 4 nchini Kenya kabla ya kusafiri Uganda kwa mechi ya marudiano itakayosakatwa Aprili 7.

Mshindi kati ya Kenya na Uganda atasonga mbele kukutana na mabingwa wa Afrika mwaka 2008 na 2012 Equatorial Guinea katika raundi ya pili mwezi Juni. Mshindi wa raundi ya pili atafuzu kushiriki Kombe la Afrika ambalo Ghana itaandaa mnamo Novemba 17 hadi Desemba 1 mwaka 2018.

Mara ya mwisho Kenya na Zambia zilikutana ni mwaka 2017 katika mashindano ya Afrika ya Kusini (Cosafa) nchini Zimbabwe. Starlets, ambayo iliakwa kushiriki makala hayo ya tano, ilitoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida kabla ya kulazwa 4-2 kwa njia ya penalti katika mechi ya kutafuta nambari tatu.