• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Wakuu wa jela wahamishwa kashfa ikizuka

Wakuu wa jela wahamishwa kashfa ikizuka

VINCENT ACHUKA na DOMINIC WABALA

SERIKALI imewahamisha maafisa wanaosimamia magereza nchini.

Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Urekebishaji Tabia, Zainab Hussein, Jumapili aliwapa maafisa hao wa magereza wiki moja kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi.

Serikali imehamisha maafisa hao huku kukiwa na madai kwamba baadhi ya wasimamizi wa magereza wamepokea hongo ili kuruhusu wahalifu sugu 120 kuachiliwa huru kupitia msamaha wa rais mwaka huu.

Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) imeanzisha uchunguzi ili kunasa maafisa waliohusika katika sakata hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na DCI uligundua kwamba wengi wa wafungwa katika orodha ya waliofaa kuachiliwa huru kupitia msamaha wa rais walikuwa wahalifu sugu ambao hawakutimiza masharti.

Idara ya DCI inayoongozwa na Bw George Kinoti imeagiza kufanywa kwa uchunguzi ili kubaini kilichosababisha wahalifu sugu kuwekwa katika orodha ya wafungwa wanaofaa kuachiliwa huru kupitia msamaha wa rais.

Kati ya wafungwa 120 waliofaa kuachiliwa huru, 82 walikuwa wafungwa wa wizi wa mabavu, 22 ni wauaji na 11 wa makosa mengineyo.

Wengi wa wafungwa walio katika orodha hiyo wana umri wa kati ya miaka 32 na 50 na kuna hofu kwamba huenda wakarejelea maisha yao ya uhalifu.

Idara ya DCI sasa inataka kamati ambayo imetwikwa jukumu la kuchunguza wafungwa wanaofaa kuachiliwa huru kupitia msamaha wa rais, kujumuisha maafisa wa DCI, Idara ya Ujasusi (NIS), afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na wizara ya Usalama wa Ndani.

Kupitia barua yake kwa Waziri wa Usalama wa Nchi Fred Matiang’i, Bw Kinoti alisema kuwa idadi kubwa ya wafungwa walio katika orodha hiyo wametekeleza makosa ya jinai.

“Tulipokea barua iliyoandikwa Mei 15, 2019 kutoka kwa Mkuu wa Sheria ikitutaka kuchunguza wafungwa 120 wanaofaa kuachiliwa huru kupitia msamaha wa rais.

“Maafisa wetu walichunguza alama za vidole za wafungwa hao 120 namna ilivyoelezwa katika barua ya Mkuu wa Sheria. Tulibaini kuwa baadhi ya wafungwa wamewahi kutekeleza uhalifu zaidi ya mara mbili,” ikasema ripoti ya DCI.

Kulingana na Sheria kuhusu Msamaha wa Rais, kamati inayochunguza wafungwa wanaofaa kuachiliwa inastahili kutumia kigezo cha umri, mazingira yaliyosababisha mhusika kutekeleza uhalifu, ikiwa mhusika alitekeleza uhalifu kwa mara ya kwanza, urefu wa kifungo, hali ya afya ya mfungwa, usalama wake katika jamii kati ya vigezo vinginevyo.

You can share this post!

Seneta apigia debe Punguza Mizigo

Jumwa apata pigo akimpigia debe mwaniaji wa udiwani

adminleo