• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Simanzi maziko ya wahanga 68 wa ajali ya mafuta yakianza TZ

Simanzi maziko ya wahanga 68 wa ajali ya mafuta yakianza TZ

NA MASHIRIKA

MAJONZI yalitanda nchini Tanzania Jumapili wakati maandalizi ya kuwazika zaidi ya watu 60 waliokufa kwenye moto uliotokea baada ya ajali ya lori la mafuta Jumamosi, yalipoanzishwa.

Rais wa Tanzania John Magufuli alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia ajali hiyo ambayo ilipelekea watu 68 kufariki na wengine karibu 70 kuachwa katika hali mahututi mjini Morogoro.

Taarifa kutoka kitengo cha Mawasiliano cha Afisi ya Rais jijini Dar es Salaam ilisema siku hiyo ya maombolezo ilianza Jumamosi na inatarajiwa kukamilika leo.

“Wakati wa maombolezo, bendera ya taifa itapeperushwa nusu mlingoti. Rais atamtuma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mjini Morogoro kumwakilisha wakati wa mazishi ya walioaga dunia yaliyoanza jana,” ikasema taarifa ya Afisi ya Rais.

Mnamo Jumamosi saa mbili asubuhi, kisa kisichotarajiwa cha moto kilitokea katika mji wa Morogoro, mita 200 kutoka kituo cha mabasi cha Msamvu.

Baadhi ya wenyeji wa Morogoro walionekana wakiwamwagia wenzao ambao walikuwa wakiteketea mchanga kama njia ya kuzima makali ya moto miilini mwao. Hakika lilikuwa tukio la kusikitisha sana ambalo halitatoka kwenye akili ya wenyeji miaka kadhaa ijayo.

Lori lililokuwa likisafirisha mafuta ya petroli kutoka Dar es Salaam hadi Mafinga eneo la Iringa, lilikuwa limeanguka baada ya kuhepa kumgomga mwendeshaji wa pikipiki kisha likagonga mti na kuangukia barabarani.

Kama kawaida kwenye ajali kama hizi, mamia ya raia walikimbilia kufyonza mafuta bila kufahamu kwamba tabia yao ingezamisha taifa hilo kwenye biwi la majonzi na maombolezo dakika chache baadaye.

Kabla ya mlipuko na moto kutokea, picha zilizopigwa zilionyesha wanaume, wanawake na watoto wakiwa wamebeba mitungi na ndoo wakiyateka mafuta kutoka kwenye lori hilo huku mengine yakimwagika chini na kuenea ardhini.

Walioshuhudia janga hilo walisimulia jinsi mafuta yalivyotapakaa ardhini na kuonekana kuzingira raia hao waliofikiria bahati imewaangukia bila kufahamu walikuwa wakihatarisha maisha yao.

“Nafikiri kila mtu alitilia maanani utekaji wa mafuta hayo na kusahau hatari iliyokuwa ikiwakodolea macho. Hii ndiyo maana wengi waliaga dunia,” akasema mwanaume kwa jina Joram ambaye alishuhudia tukio lenyewe tangu mwanzo hadi mwisho.

Watu 68 walithibitishwa kufariki na wengine 70 kuwa katika hali mahututi kwenye kisa hicho kinachoendelea kuhuzunisha raia wa Tanzania na ulimwengu mzima.

“Kilichojiri ni kwamba watu walizingirwa na mafuta yaliyotapakaa ardhini na moto ulipotokea hawangetoroka kwa urahisi. Nafikiri hiyo ndiyo sababu kuu ya kutokea kwa vifo vingi,” akaongeza Bw Joram.

You can share this post!

Jumwa apata pigo akimpigia debe mwaniaji wa udiwani

AKILIMALI: Mashine za kisasa kurahisisha kilimo

adminleo