• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Kocha wa Vihiga United aomba radhi kwa kuropokwa uwanjani

Kocha wa Vihiga United aomba radhi kwa kuropokwa uwanjani

Na CECIL ODONGO

KOCHA Mkuu wa timu ya Vihiga United Edward Manoa amemwomba radhi mwamuzi aliyechezesha mechi kati yao na Kakamega Homeboyz kwa matamshi aliyoyatoa baada ya mechi.

Akiwa amechemka kwa hasira mkufunzi huyo alimlaumu refari Andrew Juma kwa kuonea timu yake na kutoa maamuzi ya kukandamiza wachezaji wake timu hizo zilipotifuana februari 24 mwaka 2018.

Mechi hiyo iliyobatizwa ‘Western derby’ ilishuhudia Vihiga United wakikalifishwa mabao 2-1 na Kakamega Homeboyz uwanjani Bukhungu Kaunti ya Kakamega.

“Nimesikitikia kiwango cha usimamizi wa mechi  dhidi ya wapinzani wetu ambao nautaja kuwa duni.

Hamna haja ya maonevu haya hata ikiwa sisi ni wageni kwenye ligi.Lazima marefari waambiwe ukweli,” alisema kocha Manoa kwenye mahojiano ya baada ya mechi wakati huo

Akisikitia kauli yake, kocha huyo alimtakia Bw Juma usimamizi wa kuridhisha kwenye mechi atakazosimamia ligi ikiendelea na kumtaja kama mojawapo wa wamuuzi bora wanaotambuliwa hapa nchini na Shirikisho la Soka duniani FIFA.

“Nasikitia matamshi yangu na athari yake kwa taaluma yako ya kuchezesha mechi za ligi mbalimbali.Wewe ni refari anayewajibikia kazi yake vilivyo na ninaomba msamaha kutokana na kauli yangu,”  akaomba radhi kocha huyo mwenye tajriba ya miaka mingi ya ukufunzi.

Hata hivyo kumekuwa na hisia kali kutoka kwa wadau kwenye fani ya soka hapa nchini kutokana na kiwango cha marefari wanaocheza michuano ya ligi.

Kocha wa Kakamega Homeboyz Francis Baraza ni wa hivi punde kuchemkia waamuzi.

Jumapili alilamika vikali kuhusu timu yake kuonewa na refarii aliyechezesha mechi kati yao na AFC Leopards waliyopoteza 2-1 uwanjani Machakos.

 

You can share this post!

Rwanda yajiandaa kuchuana na Kenya U-20 Kombe la Afrika

Wazito FC wamridhisha kocha kwa bidii yao

adminleo