Polisi wazima wakazi kuchota mafuta Nakuru
Na PHYLLIS MUSASIA
LICHA ya mkasa wa moto kuua watu karibu 70 walioenda kuchota mafuta kwenye lori lililopata ajali Tanzania wikendi, wakazi wa Nakuru Jumatatu walijitokeza kwa wingi wakiwa na nia ya kuchota mafuta yaliyokuwa yakimwagika kwenye lori.
Raia walijitokeza wakiwa wamebeba vibuyu tayari kuchota mafuta, lakini polisi wakafanikiwa kuwazuia.
Ilibidi sehemu moja ya barabara kuu ya Nakuru kuelekea Nairobi eneo la Pipeline kufungwa baada ya kugunduliwa lori hilo lilikuwa linamwaga petroli.
Lori hilo lilikuwa likitoka Mombasa kuelekea Kampala, Uganda.
Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Nakuru, Bw Stephen Matu, alisema lori hilo lilikuwa limebeba lita 45,000 za petroli aina ya supa na tangi ambalo lilikuwa likimwaga petroli lilikuwa na takribani lita 17,000.
“Ilikuwa ni mwendo wa saa nne asubuhi dereva wa lori hilo alipogundua kuwa petroli ilikuwa ikimwagika na ikabidi aliweke kando ya barabara ili lichunguzwe,” akasema Bw Matu.
Wafanyabiashara karibu na eneo hilo waliagizwa kufunga maduka yao na kuondoka haraka iwezekanavyo.
Bi Teresia Wanjiku alisema kuwa alikuwa kwenye mstari wa mbele kuondoka dukani mwake.
Alisema hakusubiri kukumbushwa mara ya pili kwani ameshawahi kumpoteza mpendwa wake katika mkasa wa moto uliowahi kutokea nchini.
Moto mwingine sawia na wa Morogoro nchini Tanzania mnamo Jumamosi ulitokea mwaka wa 2009 katika eneo la Sachangwan, Nakuru na kuwaua zaidi ya watu 100 huku wengine wengi wakijeruhiwa vibaya.