• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
AFYA: Kukabili maumivu makali ya kichwa

AFYA: Kukabili maumivu makali ya kichwa

Na LEONARD ONYANGO

“MAUMIVU yakizidi, pata ushauri wa daktari.” Hiki ndicho kibwagizo cha matangazo ya dawa, hasa zile za kupunguza maumivu ya kichwa.

Ni vigumu kukosa tembe za kupunguza maumivu ya kichwa katika maduka mengi humu nchini kuanzia vijijini hadi mijini.

Dawa hizi hupatikana kwa urahisi na bei nafuu, hivyo watu wanazitumia kwa wingi.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa utumiaji wa dawa za kupunguza maumivu ya kichwa mara kwa mara husababisha uraibu sawa na wa mihadarati.

Mwathiriwa hawezi kulala au kufanya kazi bila kumeza tembe kadhaa za kupunguza maumivu ya kichwa au mwili.

Utumiaji wa dawa hizi kupita kiwango kwa muda mrefu hudhuru afya na hata kusababisha kifo.

Ripoti kuhusu matumizi ya dawa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN) majuzi, ilionya kuwa idadi ya watu wanaotumia dawa kiholela bila ushauri wa daktari inazidi kuongezeka duniani.

Kupunguza maumivu

Ripoti hiyo inakadiria kuwa watu 585,000 waliaga dunia kutokana na matumizi mabaya ya dawa, zikiwemo tembe za kupoza maumivu ya kichwa mwaka 2017.

Ongezeko la madhara ya tembe za kupunguza maumivu ya mwili, kumezua mjadala mkali miongoni mwa wataalamu wa afya.

Baadhi ya wataalamu wanataka bangi ihalalishwe ili madaktari waweze kuitumia kutibu maumivu ya mwili yakiwemo yale kichwa.

Wanaounga mkono pendekezo hilo wanasema kuwa dawa zinazotengenezwa kwa bangi zinaweza kupunguza maumivu bila kudhuru afya.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha McGill nchini Canada walifanya utafiti mwaka 2018 na kubaini kuwa bangi inaweza kutumiwa kama dawa ya kupoza maumivu makali ya kichwa bila kulewesha mtumiaji.

“Tulitumia mnyama kufanya utafiti huo ambapo tuligundua kwamba dawa inayotokana na bangi inaweza kuponya maumivu makali ya kichwa,” wakasema watafiti hao.

Wanaopinga kuhalalishwa kwa dawa iliyotengenezwa kwa bangi wanasema kuwa huenda hatua hiyo ikatoa mwanya kwa watu kuitumia vibaya.

Wataalamu wanashauri mtu anapotumia dawa za kupunguza maumivu ya kichwa ni sharti ameze dawa zisizo na chembechembe za ‘caffeine’ ambazo husababisha uraibu.

Kulingana na watalaamu, ikiwa maumivu ya kichwa yanajitokeza mara mbili kwa wiki, ni vyema kwenda hospitalini badala ya kumeza tembe nyingi kupita kiasi na kukugeuza mraibu.

Tayari Wizara ya Afya nchini Uingereza, imetangaza kuwa wagonjwa wa maumivu makali ya kichwa sasa hawatapewa tembe.

Badala yake, watapewa kidubwasha cha GammaCore.

Kifaa hicho hushikiliwa kwa mkono na kuwekwa shingoni. Kinatoa miale ya kielektroniki ambayo husisimua misuli na kupunguza maumivu.

Kinaweza kuponya aina zote za maumivu ya kichwa lakini sasa hospitali za Uingereza zinakitumia kuponya maumivu makali kupindukia.

Maumivu makali kupindikia ya kichwa hujitokeza kwa kushtukiza na hudumu kwa kati ya dakika 15 na sasa moja. Maumivu hayo yanaweza kujitokeza kwa zaidi ya mara mbili kwa siku.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni nchini Korea Kusini ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 40 ya waathiriwa wa maumivu makali ya kichwa wamewazia kujitia kitanzi. Baadhi ya watu waliohojiwa katika utafiti huo waliwahi kujaribu kujiua.

Mgonjwa huanza kupata nafuu dakika mbili baada ya kuweka kifaa hicho shingoni.

Kifaa hicho huenda kikapunguza matumizi ya tembe kutuliza maumivu ya kichwa.

Kiliidhinishwa na serikali ya Uingereza kutumiwa kwa matibabu 2018.

Ni kidubwasha cha kwanza kinachoshikiliwa kwa mikono kuidhinishwa ili kutibu maumivu ya kichwa.

You can share this post!

ATHARI ZA PLASTIKI: Walaji samaki wa baharini wanajaza...

MAZINGIRA NA SAYANSI: Faida tele za kuendesha baiskeli na...

adminleo