• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Waangalizi wa uchaguzi walitishwa na kuuawa, Elog yasema

Waangalizi wa uchaguzi walitishwa na kuuawa, Elog yasema

Mwenyekiti wa Elog Bi Regina Opondo. Picha/ Hisani

Na BENSON MATHEKA

WAANGALIZI wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2017 walihudumu katika mazingira magumu ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kutishwa na kuuawa, shirika moja limesema Alhamisi.

Kwenye ripoti shirika la Elections Observation Group linasema (Elog) kwamba jukumu la waangalizi katika uchaguzi halikueleweka vyema na wanasiasa na hata wanahabari

Kundi hilo linasema mazingira magumu ya kisiasa yaliathiri maandalizi ya uchaguzi na kwa sababu ya kutishwa, makundi ya waangalizi yaliondoa waangalizi katika marudio ya kura ya urais Oktoba 26 mwaka 2017.

Kulingana na kundi hilo, uadilifu wa uchaguzi huo hauwezi kuthibitishwa kwa sababu halikutuma waangalizi katika maeneo yote nchini.

Ripoti iliyozinduliwa Alhamisi inasifu mahakama kwa kujiandaa mapema kukabiliana na kesi za uchaguzi japo kulikuwa na vitisho.

Shirika hilo linataka maafisa wa usalama wapewe mafunzo maalumu kuhusu mfumo wa uchaguzi nchini kabla ya kutumwa kwenda kudumisha usalama wakati wa uchaguzi.

 

Mafunzo ya kina

Kwenye ripoti yake kuhusu uchaguzi huo, Elections Observations Group ( ELOG), linasema kwamba polisi wanafaa kupewa mafunzo ili kudumisha usalama wa kutosha kabla, kwenye uchaguzi na baada ya uchaguzi ili kulinda wapigakura na wadau wengine.

“Mafunzo ya kina kwa maafisa wa usalama wanaotumwa kudumisha usalama wakati wa uchaguzi yanafaa ili waweze kuelewa mfumo wa uchaguzi,” inasema ripoti ya ELOG.

Maafisa wa polisi walilaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakikabiliana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.Watu kadhaa wakiwemo watoto waliuawa kwenye ghasia hizo.

Ripoti ya ELOG inasema kwamba maafisa wa usalama wanaotumwa kukabiliana na ghasia wakati wa uchaguzi wanafaa kuwa huru na kutoengemea upande wowote wakitekeleza majukumu yao.

“Wanafaa kutekeleza majukumu yao kwa utaalamu wa hali ya juu, uadilifu, uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu,” inaeleza ripoti ya kundi hilo ambalo ni muungano wa mashirika kadhaa ya kijamii na yasiyo ya kiserikali nchini.

 

Watu 67 waliuawa

ELOG linasema kwamba watu 67 waliripotiwa kuuawa baada ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wafuasi wa upinzani.

“ELOG liligundua kuwa mtindo huu wa kutumia nguvu kupitia kiasi dhidi ya waandamanaji katika ngome za upinzani uliendelea hadi na baada ya marudio ya kura ya urais Oktoba 26 2017,” inaeleza ripoti ya kundi hilo.

Kulingana na ripoti hiyo, waangalizi wa uchaguzi, walitishwa, kunyanyaswa na hata kuuawa wakitekeleza kazi yao.

Mwenyekiti wa ELOG, Bi Regina Opondo alisema mwangalizi mmoja wa kundi lao, Vincent Omondi aliuawa katika hali ambayo haikueleweka.

“Matukio kama haya yalifanya vikosi vya usalama kulaumiwa kwa kutekeleza majukumu yao kwa ubaguzi na kulenga wafuasi wa NASA hata walipokuwa wakiandamana kwa amani.

Kulikuwa pia na madai kwamba polisi walitumia makundi yenye silaha kukabiliana na waandamanaji wa NASA,” inaeleza ripoti hiyo.

“ELOG iligundua kuwa hakukuwa na uwajibikaji na uwazi kutoka kwa polisi kuhusu majukumu yao. Pia, mashirika yanayofaa kuhakikisha polisi wanatenda kazi yao kisheria hayakufanya kazi yao inavyofaa na kwa hivyo polisi walivunja haki za binadamu bila kujali sheria,” inaeleza ripoti hiyo yenye anwani, One Country, Two Elections, Many Voices.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Nairobi Alhamisi, Askofu Alfred Rotich wa kanisa Katoliki alilaumu wanasiasa kwa kupuuza ushauri wa tume kadhaa zilizopendekeza jinsi ya kuepuka ghasia katika uchaguzi nchini.

“Ghasia zilizoelekezewa Wakenya baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 hazikufaa,” alisema Askofu Rotich.

You can share this post!

Aibu kwa viongozi wa Laikipia wanafunzi kutumia mawe kama...

Vijana tumieni vyema Sh200 bilioni za serikali kujinufaisha...

adminleo