• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wito maoni ya BBI na ‘Punguza Mizigo’ yaunganishwe

Wito maoni ya BBI na ‘Punguza Mizigo’ yaunganishwe

Na SAMUEL BAYA

WITO umetolewa kuunganisha mapendekezo ya vuguvugu la ‘Punguza Mzigo Initiative’ na lile la ‘Building Bridges Initiative (BBI) ili kujumuisha maoni yote katika kapu moja la kurekebisha katiba.

Wachanganuzi wa siasa kwenye mahojiano waliyofanya jana na Taifa Leo walisema, litakuwa jambo la busara maoni hayo yote yakiwekwa pamoja kisha kupimwa na kuchagua yale ya kujumuishwa katika marekebisho yanayopiganiwa kwa sasa.

Kwenye mahojiano yetu, afisa wa zamani wa mawasiliano katika ubalozi wa Amerika, Bw Kazungu Katana alisema mapendekezo yote ya mavugvugu hayo yanafaa kuwekwa katika kapu moja kisha kuchuja yale ambayo Wakenya wanataka yawekwe katika katiba.

“Kuwa na sauti hizi mbili pamoja na ile nyingine ya magavana ni jambo la busara na ambalo linahitaji kutiliwa maanani zaidi. Naamini tukichanganya maoni haya yote kwa mpigo, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kufaulu,” akasema Bw Katana.

Naye msomi na mdadisi wa masuala ya siasa Prof Hassan Mwakimako alisema juhudi za kurebekisha katiba zinaongozwa na viongozi ambao wanajiangalia wao wenyewe badala ya kuangalia maslahi ya Wakenya kwa jumla.

Aidha, Prof Mwakimako hata hivyo alikiri kwamba kuna mianya katika katiba ambayo inafaa kufanyiwa mabadliko lakini jambo hilo linaweza kutekelezwa vyema kwa kuwashirikisha Wakenya wote wala sio viongozi wachache.

“Ukisikiliza kwa makini nyendo za viongozi wetu na hata matamshi yao jukwaani, utapata picha kamili kwamba kuna tatizo mahali. Hii ni kwa sababu wanajiangalia wao na kutaka kuunda katiba ambayo itakuwa ikigawanya mamlaka badala ya kuangalia ni jinsi gani mabadiliko hayo yataimarisha hali ya maisha ya Wakenya wa kawaida mitaani,” akasema Prof Mwakimako.

Akiongea na Taifa Leo, mhadhiri katika chuo kikuu cha Pwani Priof Halim Shaurui alisema mapendekezo ya wanasiasa huenda yakawachanganya Wakenya wa kawaida.

“Umefika wakati wanasiasa hawamfanyii mema raia wa kawaida. Leo kuna Punguza Mizigo, BBI na Ugatuzi Initiative. Je haya yote yanamfaa vipi Mkenya wa kawaida,” akahoji Bw Shauri.

Alisema ni vuguvugu la Punguza Mzigo Initiative linaloongozwa na Bw Ekuru Aukot ambalo lilitumia njia ya kisheria kutaka mabadiliko ya katiba na wala sio kundi la BBI au Ugatuzi Intiative.

“Ukiangalia kundi la BBI, lilianzishwa kufuatia mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga lakini halina mashiko yoyote kisheria. Bw Aukot ndiye aliyeamua kufuata njia sahihi ya kutafuta sahihi za Wakenya zaidi ya millioni moja kama inavyotaka sheria na akafaulu,” akasema Prof Shauri.

Wakenya katika siku za hivi punde wameshuhudia mchakato mkubwa wa kutaka kuifanyia katiba mabadiliko. Tayari, vuguvugu la Punguza Mizigo limekuwa likizunguka katika kaunti mbalimbali likitaka uungwaji mkono na mabunge ya kaunti ili kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko ya kikatiba.

You can share this post!

Mwanaume afariki baada ya kuburudika kingono na mjane

Polisi waendesha msako wa walanguzi wa dawa Pwani

adminleo