ODONGO: FKF izingatie utaalamu kabla ya kuteua kocha mpya
NA CECIL ODONGO
SHIRIKISHO la Soka Nchini (FKF) linafaa kuhakikisha kwamba kocha mpya atakayeteuliwa kuongoza Harambee Stars ana rekodi ya ufanisi kwenye taaluma ya ukufunzi.
Hii ni baada ya aliyekuwa kocha Sebastien Migne mnamo Jumatatu wiki hii kuafikiana na FKF kutamatisha kandarasi yake iliyokuwa imesalia miaka miwili ikamilike.
Migne aliagana na Stars baada ya kuiongoza kushiriki kwa mara ya pili kwenye Kombe la Bara Afrika (AFCON) iliyokamilika mwezi jana nchini Misri.
Stars hata hivyo ilishindwa kupita hatua ya makundi kwenye kipute hicho na hivi majuzi pia ilibanduliwa kwenye mashindano ya CHAN yanayoshirikisha wachezaji wa klabu za nyumbani pekee.
Ingawa mjadala umechipuka kuhusu iwapo kocha mpya au wa kigeni ndiye anafaa kutwaa nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Mfaransa huyo, ni vyema atakayeteuliwa, awe wa kigeni au kutoka nchini, awekewe malengo ya kutimiza kwenye mkataba wake.
Japo sipingi raia wa kigeni kupewa kazi hiyo, FKF imekuwa na tabia ya kukimbilia makocha hao kisha kuwalipa mishahara mikubwa ilhali hawavumishi timu kwenye mashindano hata yasiyokuwa na ushindani mkali kama ya kuwania ubingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Vilevile inafaa makubaliano yatakayowekwa na kocha huyo yabainishe wazi kwamba atatimuliwa kazini iwapo hatatimiza malengo aliyowekewa, ndipo awe na msukumo wa kulenga ufanisi kwenye utendakazi wake.
Kabla ya kung’atuka, Migne aliwaeleza wanahabari kwamba shirikisho lingejuta iwapo lingempiga kalamu kwa kuwa mkataba wake haukuwa umekamilika, na lingelazimika kumlipa fedha nyingi jinsi ilivyo kwenye mkataba wake. Kiburi kama hiki kitazimwa tu kupitia maelewano na masharti makali ya utendakazi.
Jambo jingine ambalo linafaa kuzingatiwa ni kiwango cha mshahara kwa kocha mpya.
Ni wazi kwamba makocha wa kigeni hulipwa fedha nyingi ambazo huwa ni mzigo kwa shirikisho lenyewe kuliko makocha wa hapa Kenya.
Hii ndiyo maana bado kuna kesi katika mahakama ya kutatua mizozo ya michezo zilizowasilishwa na waliokuwa makocha Bobby Williamson na Adel Amrouche wanaodai FKF mamilioni ya fedha kwa kukosa kulipwa mshahara walipohudumia Stars kabla kandarasi zao kukatizwa.
Ni kutokana na hili ambapo shirikisho lafaa kumtafuteakocha wa kulipwa fedha za wastani na hayo yanakiliwe kwenye makubaliano kwamba kiasi hicho kitaongezwa hadi kiwango fulani iwapo ataongoza timu kung’aa kwenye mechi mbalimbali.
Kocha mpya pia apewe uhuru wa kuwachagua wachezaji jinsi anavyotaka bila kuingiliwa.