• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
TAHARIRI: Rais aongee na vinara wa kaunti kwa dharura

TAHARIRI: Rais aongee na vinara wa kaunti kwa dharura

NA MHARIRI

Kuna msemo usemao, wapiganapo fahali wawili, iumiayo ni nyasi. Na yamkini wafanyakazi katika kaunti 20 wamesadiki maana ya msemo huo baada ya kukosa mshahara wao wa mwezi jana.

Wakati umewadia kwa magavana, maseneta, Wabunge na Wizara ya Fedha kufanya kikao cha dharura kutafuta suluhu kwa vuta nikuvute inayoendelea na ambayo imekwamisha huduma mashinani.

Wafanyakazi husika wamekuwa na subira kwa muda mrefu. Na sasa ni wazi kwamba, huenda operesheni katika kaunti hizo zikakwama pakubwa ikiwa wafanyakazi hao hawatalipwa kwa haraka.

Wizara ya Fedha inapasa kutoa pendekezo la kupatanisha pande husika ili kumaliza mtafaruku huu mkubwa ambao umeibua kilio katika familia nyingi. Kwa mfano, Kati ya Sh335 bilioni ambazo seneti inapendekeza zisambazwe kwa kaunti, Bunge la Kitaifa linaweza kuongeza pendekezo lao la Sh316b hadi Sh325b kwa moyo wa nipe nikupe.

Ukweli ni kwamba, serikali za kaunti zilitwaa majukumu mengi chini ya mfumo wa ugatuzi. Huduma muhimu kama vile afya, kilimo, maji na nyinginezo sasa zimo mikononi mwa magavana. Haifai serikali kuu kuendelea kubaki na asilimia kubwa ya mapato ya nchi ilhali mengi ya majukumu ya utawala yamegatuliwa.

Ni kinaya kwamba, licha ya msukosuko wa sasa, huduma katika serikali kuu zinaendelea kama kawaida. Kama ilivyo mazoea ya utawala wa sasa, lile ambalo linakinzana na matakwa yao linapuuzwa.

Maafisa wa serikali walichukua njia ya mkato na kusambaza pesa kwa wizara mbalimbali kabla ya mswada wa ugavi wa fedha za serikali kupitishwa.

Kimsingi, pesa hizo zilisambazwa kinyume cha sheria. Je, hali ingekuwaje iwapo Rais, Mawaziri na watumizi wa ngazi za juu wangekosa mshahara na marupurupu yao kutokana na mgogoro huu?

Tayari, wauguzi wametangaza kwamba watagoma endapo hawtalipwa mishahara yao haraka iwezekanavyo. Wahudumu wengine katika idara mbalimbali za kaunti wametishia kususia kazi vile vile.

Ni nani atawalaumu? Wengi wameelezea masaibu wanayopitia kwa sasa huku baadhi wakilazimika kushiriki mchezo wa paka na panya na wenye nyumba wanakoishi.

Baadhi hata wamekosa chakula. Yote hayo yanaendelea huku wale wanaosimamia ugavi wa mapato ya nchi wakishiriki kwenye vita vya ubabe.

Rais Kenyatta anapasa kubatilisha kauli yake ya awali kwamba serikali haina pesa, aandae kikao cha pamoja na wahusika wote ili jawabu la kudumu lipatikane. Huo ndio uongozi bora.

You can share this post!

ODONGO: FKF izingatie utaalamu kabla ya kuteua kocha mpya

Uchafuzi wa mito huanza kwenye chemchemi

adminleo