Uchafuzi wa mito huanza kwenye chemchemi

NA WAANDISHI WETU

KULINGANA na uchunguzi wa Taifa Leo, ambapo waandishi wetu walifuata Mto Nairobi kutoka chemichemi yake katika Kaunti ya Kiambu hadi Bahari Hindi, mto huo umechafuka zaidi na unaendelea kuchafua kila mahala unapopitia kuungana na mito mingine.

Mto huo unaanza katika Kinamasi cha Ondiri katika Kaunti ya Kiambu. Mara unapoanza kutiririka uchafuzi wake unaanza kutokana na shughuli za kilimo.

Kisha unaanza kuchanganyika na maji taka kutoka makazi mengi maeneo unakopita na unapofika Nairobi unachafuka zaidi kwa maji taka, uoshaji magari na umwagaji wa taka za viwandani.

Mto huo kisha unajiunga na mito mingine kama vile Mto Ngong unaopitia viwandani na mitaa ya mabanda ya Kibera na Mukuru huku taka zikiendelea kumwagwa ndani yake, ambao pia umechafuka. Unabeba uchafu zaidi unapopita karibu na jaa la Dandora.

Mito hii inapoungana huwa sio mito tena mbali mrundiko wa uchafu wa viwandani, miili ya watu waliokufa, uchafu kutoka hospitali, mabaki ya kemikali na dawa za kilimo, plastiki, mafuta yaliyotumika ya magari, chupa na vyuma kuukuu.

Kwenye shughuli iliyofanyika majuzi ya kuosha mto huo jijini Nairobi, miili 14 ya binadamu hasa vijusi ilipatikana imefungwa kwa karatasi za plastiki.

Kutoka Nairobi mtiririko huu wa mauti unaingia Kaunti ya Machakos na kumwaga sumu yake katika Mto Athi River, ambako unakusanya uchafu zaidi kutoka viwanda vya saruji vya Mavoko kabla ya kuingia tena Kaunti ya Kiambu upande wa chini ambapo sumu zaidi kutoka viwanda vya Thika inamwagwa.

Uchafu huu unajionyesha katika Maporomoko ya 14 Falls kutokana na povu jingi na maji ya rangi nyeusi.

Unapofika Thika, wenye mashamba ya nanasi na maua wanatumia maji haya yenye sumu kunyunyizia mazao yao.

Baada ya kutoka Kiambu unarudi Machakos hadi Makueni na Kilifi.

Katika Kaunti ya Makueni, ujenzi wa bwawa la Thwake unaendelea ambapo kiasi kikubwa cha maji kitakuwa kikitoka Mto Athi, ambao tayari umejaa uchafu.

Katika Kilifi, maji haya yanatumika katika mradi wa kilimo wa Galana Kulalu kabla ya kumwaga uchafu huo Bahari Hindi.