• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
Harambee Starlets kuvaana na Ethiopia kirafiki

Harambee Starlets kuvaana na Ethiopia kirafiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya alamaarufu Harambee Starlets imepata mechi ya kujipima nguvu kabla ya kuvaana na Malawi katika mechi ya kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2020.

Starlets itajipima nguvu dhidi ya Ethiopia uwanjani Kenyatta mjini Machakos mnamo Agosti 17, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilitangaza Jumanne.

Warembo wa kocha David Ouma (pichani) watatangulia kuzuru Malawi mnamo Agosti 28 kabla ya kualika timu hiyo kwa mechi ya marudiano mnamo Septemba 1 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

Starlets ilianza kambi ya mazoezi Agosti 12. Itakutana na Malawi katika raundi ya pili baada ya kupewa tiketi ya bwerere kutokana na kukosa mpinzani katika raundi ya kwanza.

Malawi ilianzia kampeni yake katika raundi ya kwanza kwa kuaibisha Msumbiji kwa jumla ya mabao 14-1 mwezi Aprili baada ya kuichabanga 11-1 jijini Blantyre na kuilemea 3-0 jijini Maputo.

Mshindi kati ya Kenya na Malawi atamenyana na mshindi kati ya Ghana na Gabon katika raundi ya tatu kati ya Septemba 30 na Oktoba 4. Kutakuwa na raundi mbili zaidi kabla ya timu kufika Olimpiki.

Kuhusu mechi kati ya Kenya na Ethiopia ni kuwa majirani hawa wanafahamiana. Starlets ilichapa Ethiopia 3-2 katika nusu-fainali ya soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mwaka 2016 nchini Uganda kabla ya kusimamishwa na Tanzania 2-1 katika fainali.

Zilipokutana katika makala yaliyofuata, ambayo yalifanyika mwaka 2018, Kenya ililazwa 1-0.

You can share this post!

Wito afisi ya kijinsia ifufuliwe Baringo

Mariga aisaidia Mabazenga FC kunasa taji la Kriss Darling

adminleo