Duale: Uchaguzi mkuu 2022 ni kinyang'anyiro cha Ruto na Raila
Na SAMMY WAWERU
JUBILEE Party (JP) kingali imara na viongozi wake wako pamoja, amesema Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale.
Duale pia amesema Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto wanafanya kazi kwa pamoja na kushauriana kama ilivyokuwa awali.
Jumanne usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, kiongozi huyo alipuuzilia mbali madai kuwa uhusiano baina ya Rais na naibu wake ni wa kutiliwa shaka, akitaja tetesi hizo kama “zinazopotosha”.
Alisema miungano inayoshuhudiwa nchini ikiegemea upande mmoja au mwingine wa viongozi ni ya kibinafsi na kwamba haihusishwi kwa vyovyote na JP.
Bw Duale alikuwa akizungumza kuhusu kundi la ‘Tangatanga’ linalohusishwa na Naibu Rais Dkt Ruto, Kieleweke; Rais Kenyatta, Inua Mama na Embrace ambacho ni kikundi kinachodai kuhamasisha maridhiano kati ya Rais na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Hiyo miungano haihusishwi na Jubilee na hutaniona nikiegemea muungano wowote,” alisema.
Salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Bw Raila maarufu kama Handisheki Machi 2018, zimekuwa zikikosolewa na wandani wa Dkt Ruto wakizitaja kama njama ya kuzima azma yake kumrithi Rais 2022.
Ni katika jukwaa la mahojiano hayo ambapo Duale alisema uchaguzi wa 2022 utakuwa kati ya vigogo wawili.
“Utakuwa wa farasi wawili; William Ruto na Raila Odinga, wengine ni punda (kauli inayotumiwa na wanasiasa na wachanganuzi kuashiria wangombeaji wenye ushindani mkali kwenye uchaguzi). Ni wazi nitamuunga Bw Ruto,” Duale alieleza.
Alisema Rais Kenyatta ambaye ndiye kiongozi wa JP ataunga mkono mgombea atakayeteuliwa na wajumbe wa chama hicho, kwenye uteuzi wa kitaifa.
Bw Duale pia alisema madai kuwa Rais Kenyatta, Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Seneta wa Bungoma na ambaye ni kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na kiongozi wa Kanu Gideon Moi ambaye pia ni Seneta wa Kaunti ya Baringo, huenda wakaunda muungano utakaoamua atakayerithi Ikulu 2022 “ni habari bandia.”
Vigezo
Kiongozi huyo wa wengi bungeni alisema anaunga mkono mchakato wa kura ya maamuzi kubadilisha Katiba kwa vigezo vitatu pekee; ushirikishi wa kila tabaka kwenye uongozi, kuzika katika kaburi la sahau ukabila na kuondoa ghasia kila mwaka wa uchaguzi.
Duale ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais Dkt Ruto, ambaye amekuwa akikosoa mchakato huo. Ruto anasema ataunga mkono kura ya maamuzi kurekebisha katiba iwapo italenga kuondolea mwananchi mzigo, ila si ya kubuni nyadhifa za wanasiasa, hasa walioanguka kwenye uchaguzi.
Kufuatia Handisheki, kamati ya kiufundi-BBI iliundwa ili kukusanya maoni ya wananchi katika mjadala mzima wa kuunganisha taifa. Inatarajiwa kutoa ripoti ya mapendekezo yake mwezi Oktoba mwaka huu, ikidaiwa huenda ikapendekeza kuandaliwa kura ya maoni kubadilisha katiba.