Habari

Kuppet yataka ihusishwe kikamilifu katika utekelezaji CBC

August 14th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

CHAMA cha Walimu wa Sekondari na Taasisi za Mafunzo (Kuppet) kimetaka kihusishwe katika utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu unaojikita katika uamilifu, Competency Based Curriculum (CBC).

Katika kikao na wanahabari Jumanne, chama hicho kilimlenga Waziri wa Elimu Prof George Magoha, ambapo wanachama walisema kuwa japokuwa wanaunga mkono mfumo huo wa elimu, wametengwa katika hatua hiyo muhimu.

“Wamewapuuza walimu katika utekelezaji wa mfumo huo na badala yake kuwachagua wanakamati kutoka vitengo mbalimbali ambapo baadhi yao hawana tajriba na uelewa wa masuala ya elimu,” alisema Naibu Mwenyekiti wa Kuppet Bw Julius Korir.

Wanachama wa Kuppet kwenye kikao cha kuwahutubia wanahabari Agosti 13, 2019, jijini Nairobi. Picha/ Magdalene Wanja

Bw Korir aliongeza kuwa muungano huo unatarajia maombi yao kujibiwa kwa upesi kwani tayari Kuppet imehusika katika ukarabati wa mtaala uliopita.

“Hapo awali tumeshauriana na washikadau katika mfumo huo mpya lakini kwa sasa tungetaka mambo yaimarishwe zaidi ili muungano huu uwakilishwe katika kamati hiyo ya utekelezaji,” akasema Bw Korir.

Makubaliano ya CBA

Katibu wa Kuppet, Akelo Misori alisema kuwa muungano huo tayari umeanza mazungumzo ya kuanza upya (CBA) itakayawafaidi walimu katika mazingira yao kazini.

“Mazungumzo hayo yanatarajiwa kushika kasi kuanzia Agosti 22,” akasema Bw Misori.

Baadhi ya maswala yatakayojadiliwa ni pamoja na bima ya afya, marupurupu ya nyumba na mishahara ya walimu wa kitengo cha chini.