NDIVYO SIVYO: Mkataba na maktaba hayalandani kimaana, yanakaribiana kisauti tu
Na ENOCK NYARIKI
KATIKA kikao kimojawapo kuhusu kazi na makubaliano ya kazi yenyewe, bwana mmoja ambaye ushawishi wake ulikuwa muhimu sana katika masuala hayo mawili hakuwa na budi kuuliza kuhusu maana ya neno mkataba lilivyotumiwa na mmoja wa wataalamu wa Kiswahili na jinsi linavyotofautiana na mahali pa kuhifadhi vitabu.
Kauli hiyo iliwachekesha wakereketwa wengine wa lugha ya Kiswahili ambao walihudhuria kikao hicho.
Waama, maneno mawili tuliyoyataja yanakurubiana kwa njia nyingi hivi kwamba mtu anaweza kuyachukulia kuwa mamoja. Kwanza, yana asili moja. Pili, yanakaribiana kimatamshi na kiumbo hivi kwamba mtu anahitaji tu kuichopoa sauti ‘‘a’’ inayojiri baada ya “m” kwenye neno maktaba na kuihamishia kwa “k” ili kulipa neno lenyewe umbo sawa na neno la kwanza. Sasa tujadili maana za maneno hayo na jingine linalokaribiana nayo.
Teknolojia inaelekea kupanua maana ya maktaba. Licha ya hapo awali ambapo maktaba ilijulikana kuwa ni nyumba au chumba kilichotumiwa kuhifadhi vitabu ili watu wavifikie kwa urahisi na kuvisoma au kuviazima, siku hizi kuna malori yanayotoa huduma sawa na hizo.
Kwa hivyo, neno hilo linaweza pia kuelezewa kuwa ni vitabu vilivyokusanywa kwa minajili ya kusomwa na pengine kuazimwa. Fasili ya pili ya neno hilo haijazingatia dhana ‘chumba’ au ‘nyumba’.
Nimetumia kiambishi {i} kurejelea neno maktaba kinyume na maoni ya wataalamu wengine kuwa neno hilo liko katika ngeli ya YA-YA. Waama hili ni suala la mjadala ambalo huenda mwafaka usifikiwe katika siku za karibuni.
Hata hivyo, tuseme kuwa maktaba ni nomino inayoweza kuhesabiwa yaani tunaweza kusema maktaba moja, mbili, tatu n.k tofauti na nomino za wingi kama vile maji, maziwa, mafuta na mate ambazo haziwezi kuhesabiwa.
Hata hivyo, tulivyotangulia kusema, hili ni suala la mjadala ambalo si kiini cha mjadala wetu.
Mfanyakazi katika maktaba
Neno jingine ambalo lina uhusiano na maktaba ni mkutubi.
Mkutubi ni mfanyakazi katika maktaba anayehusika na mambo ya vitabu moja kwa moja.
Moja kati ya huduma nyingi za mkutubi ni kuwasaidia watu kuvifikia vitabu au majarida wanayoyahitaji kwa urahisi.
Kulingana na Kamusi Elezi ya Kiswahili, neno mkataba lina maana ya makubaliano yafanywayo baina ya watu, nchi au kampuni mbili yakarasmishwa kwa kuandikwa na kutiwa saini ili yasivunjiliwe mbali bila kujali.
Neno hilo lilipotumiwa katika muktadha nilioutaja katika utangulizi wa makala lilikuwa na maana ya makubaliano ya kazi.
Alhasili, mkataba na maktaba ni maneno yenye maana tofauti licha ya kukaribiana kimatamshi.