• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Kaunti kutoa msimamo wao kuhusu ‘Punguza Mizigo’

Kaunti kutoa msimamo wao kuhusu ‘Punguza Mizigo’

NA CECIL ODONGO

MUUNGANO wa Mabunge ya Kaunti (CAF) Alhamisi utatangaza msimamo wake ikiwa yataunga au kupinga mswada wa Punguza Mizigo baada ya kupokea ripoti ya mawakili waliokuwa wakiudurusu mswada huo.

Spika wa Kaunti ya Kajiado Johnson Osoi jana alisema kwamba, muungano huo ulikuwa umewateua mawakili wawili kusoma na wanatarajiwa kuwasilisha ripoti ambayo itaonyesha msimamo wao rasmi kuhusu mswada huo.

“Punde tu baada ya Punguza Mizigo kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tuliwateua mawakili wawili shupavu ambao watatukabidhi ripoti yao Alhamisi. Baada ya hayo, tutatoa msimamo rasmi kuhusu mswada huo ambao utakumbatiwa na kaunti zote 47,” akasema Spika huyo wa Kajiado.

Bw Osoi ambaye jana alimkabidhi Spika wa Nyandarua Wahome Ndegwa wadhifa wa uenyekiti wa CAF, pia alilalamikia hali ya sasa ya huduma muhimu kukatizwa katika kaunti na kulaumu Bunge la Kitaifa kuhusiana na utata kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato.

“Tunataka mwongozo ubuniwe ili pesa ambazo zinakuja kwa kaunti zisiamuliwe na watu wachache. Ni kinyume cha sheria kwa bunge la kitaifa kupitisha mswada wa ugavi wa mapato bila kuhusisha asasi nyingine,” akaongeza.

Mjadala kuhusu mswada wa Punguza Mizigo unaodhaminiwa na Kinara wa Thirdway Alliance, Ekuru Aukot, sasa unatarajiwa kurejelewa na mabunge ya kaunti zote 47 baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na mwanasiasa wa Kiambu David Ngari Kariuki.

Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia ambaye aliwakilisha Baraza la Magavana pia alilamikia kudorora kwa huduma kwenye kaunti akiomba bunge na seneti kupatana na pia kuomba fedha za ugatuzi ziongezwe. Bw Kimemia pia alisema wanachama wa baraza hilo bado wanashauriana na watatoa msimamo wao kuhusu Punguza Mizigo huku akisema, hawawezi kusalia kimya kuhusu mswada huo ambao umepingwa na vyama vikuu nchini.

Bw Ndegwa aliahidi kuongoza vyema muungano huo kufikia malengo yake ya kuhakikisha rasilimali zaidi zinatengewa ugatuzi na magavana wanazitumia kwa miradi ifaayo.

Maafisa wengine waliochaguliwa ni Florence Mwangangi (Naibu Mwenyekiti), Samwel Chepkwony (Katibu), Florence Oile (Katibu Mtendaji) na Ahmed Ibrahim Abbass kama Mweka hazina.

You can share this post!

Wadau kuandaa kikao kutatua migogoro kuhusu ukuzaji miraa

Mbunge kujenga vyoo vipya kuokoa shule

adminleo