Sh82 bilioni za ujenzi wa Bwawa la Thwake hatarini kupotea
Na PAUL WAFULA
HUENDA Kenya ikapoteza Sh82 bilioni katika ujenzi wa Bwawa la Thwake, Kaunti ya Makueni baada ya kubainika litategemea maji yenye sumu kutoka Mto Athi.
Chanzo cha pili cha maji ya bwawa hilo kitakuwa Mto Thwake ambao hukauka majira ya kiangazi, hivyo kufanya iwe vigumu bwawa hilo kuwa na maji ya kutosha.
Kulingana na waziri wa maji wa Kaunti ya Makueni, Robert Kisyula, iwapo suala hilo la uchafuzi wa Mto Athi halitatatuliwa haraka, mradi huo utaishia kuwa kazi bure.
Kulingana na wataalamu, itabidi bwawa hilo kugeuzwa kuwa la maji taka iwapo hatua hazitachukuliwa kukomesha uchafuzi wa Mto Athi.
Bwawa hilo ambalo likikamilika litakuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki na lenye ukubwa mara 10 ya lile la Ndakaini, linafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Kenya.
Kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo, Mto Athi una madini sita hatari kwa afya ya binadamu, viini vya bakteria na kemikali zenye sumu, na iwapo maji hayo yatatumiwa katika Bwawa la Thwake basi itakuwa sawa na kuwaroga mamilioni ya wakazi watakaotumia maji hayo.
Wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi walipata kuwa maji ya mto huo yana madini yanayosababisha maradhi ya kansa, kupumua na kuharibu neva.
Bwawa hilo linalotarajiwa kukamilika Desemba 2022 lilipangiwa kusaidia kuimarisha kilimo cha kunyunyizia maji katika eneo la Ukambani na Pwani, pamoja na matumizi ya nyumbani kwa binadamu na mifugo katika kaunti za Kitui na Makueni.
Maji yake pia ndiyo yamepangiwa kutumika katika mji wa tekinolojia wa Konza pamoja na kuzalisha megawati 23 za stima.
Tayari ubadilishaji wa mkondo wa maji wa Mto Athi umeanza ili kuelekeza maji hadi bwawa hilo.
“Watu wanaotumia maji maeneo ya juu hawajali maslahi ya wale wa chini. Tusiporekebisha hali tutaangamiza watu wetu. Maradhi ya kansa na kupumua yameongezeka maeneo ya mashambani kutokana na uchafuzi unaoendelea Nairobi,” akasema Gavana Alfred Mutua wa Machakos.