Michezo

WANYAMA: Ni kama mazungumzo baina ya Galatasaray na Spurs hayajapiga hatua

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

HUKU Wakenya wakiendelea kukesha kujua nyota wao Victor Wanyama atasalia jijini London ama ataelekea Uturiki, Galatasaray huenda imetoa ishara mazungumzo na Tottenham Hotspur hayajapiga hatua kwa sababu inatafuta Steven Nkemboanza Mike Christopher Nzonzi.

Tovuti ya RomaPress imeripoti kuwa Galatasaray imethibitisha inazungumza na waajiri wa kiungo huyo mkabaji wa klabu ya AS Roma nchini Italia. Nahodha wa Harambee Stars Wanyama, ambaye hatakikani Spurs pia ni kiungo mkabaji. “Galatasaray imetangaza kupitia mtandao wake rasmi wa Twitter kuwa inataka kuchukua Nzonzi kutoka Roma kwa mkopo,” tovuti hiyo imesema Jumatano.

Imeongeza kuwa mazungumzo kati ya Galatasaray na Roma yamepiga hatua kubwa na “inatarajiwa kuwa Mfaransa huyo atajiunga na klabu hii kutoka jijini Istanbul saa chache zijazo kwa mkopo.”

Ikiwa Nzonzi,30, ambaye ana asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ataachiliwa na Roma kwa mkopo, basi huenda Galatasaray ikafunga mlango kwa Wanyama ambaye uvumi umeenea sana kuwa Tottenham inatamani sana kumuuza.

Klabu za Bournemouth, West Ham, Brighton, Wolves, Sheffield United na waajiri wake wa zamani Southampton walisemekana wanamezea mate Wanyama, lakini hakuna aliyewasilisha ombi kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uingereza kilipofungwa Agosti 9.

Wanyama, ambaye aling’ara katika msimu wake wa kwanza Spurs mnamo 2016-2017, alisumbuliwa na majeraha msimu 2017-2018 na tena 2018-2019 kiasi cha Spurs kuona mchango wake timuni ni mdogo sana na hivyo kumweka sokoni.

Wanyama pia amehusishwa na waajiri wake wa zamani Celtic nchini Scotland.

Vipindi vya uhamisho nchini Uturuki na Scotland vinafungwa mapema Septemba kwa hivyo chochote chawezekana kuhusu uhamisho wa Wanyama kabla ya wakati huo.