• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Watu 10 wahojiwa kuhusiana na kisa cha ufukuaji mwili Butere

Watu 10 wahojiwa kuhusiana na kisa cha ufukuaji mwili Butere

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

WATU 10 wanazuiliwa huku wakihojiwa na ofisi ya Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) mjini Butere, Kaunti ya Kakamega baada ya maiti kufukuliwa kijijini Eburinde, Ituti.

Mwendazake Bw Martin Alukoye, aliyekuwa akifanya kazi katika serikali ya kaunti chini ya mpango wa kuwainua vijana na akina mama alikufa maji Agosti 7, 2019, na maiti yake ikazikwa usiku wa Agosti 12.

Familia yake imesema alikuwa na matatizo ya kiafya na alikufa baada ya kutumbukia mtoni wakati akivuka mto Eburinde.

Alizikwa akiwa na sare za huduma kwa kaunti.

Maofisa kadha wa serikali ya kaunti walivamia boma lao na kuifukua maiti kuchukua sare.

Ni hatua iliyoibua hisia na manung’uniko miongoni mwa jamaa za marehemu na watu wengine katika jamii.

Leo Alhamisi maafisa wa polisi wameita baadhi ya wanafamilia, naibu chifu wa eneo na maafisa kadhaa katika serikali ya kaunti waliohusika katika ufukuaji wa mwili.

Haya yamethibitishwa na naibu kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Butere, Bw Julius Achuka.

“Tunarekodi taarifa kutoka kwa watu 10 kuhusiana na ufukuaji wa mwili ambao haukuzikwa kwa kufuata utaratibu unaofaa,” amesema Achuka.

Watu hao ni maafisa watano kutoka kwa serikali ya kaunti, wanne ni wafiwa katika familia na naibu chifu wa eneo.

Amesema uchunguzi wa kina utafanywa kuhusiana na suala hilo na watakaopatikana na hatia ya ‘kuvuruga maiti’ watafikishwa mahakamani.

Ameambia wanahabari kwamba hawajabainisha ikiwa kulikuwa na agizo la mahakama kuruhusu ufukuaji maiti.

“Tumeanza uchunguzi, lakini hatujabainisha ikiwa kulikuwa na agizo la mahakama kutoa idhini ya ufukuaji kaburi kuufikia mwili wa marehemu,” amesema Achuka akiwa katika kituo cha polisi cha Butere.

Nduguye marehemu, Bw Patrick Alukoye, amesema maofisa wa kaunti walianika sare hiyo kwa mti karibu na kaburi na kuacha hapo mavazi hayo.

“Mavazi hayo yaliachwa kwa mti kwa siku mbili kabla ya kuchukua Jumatano, Agosti 14, 2019, walipotambua kwamba tulikuwa tumeripoti suala hilo kwa polisi hapa Butere,” amesema Bw Alukoye.

 

You can share this post!

Macho kwa Chager madereva 23 wakiwania taji la Kilifi Rally

Van Dijk awania kuwa Mwanasoka Bora Ulaya 2019 dhidi ya...

adminleo