Michezo

Van Dijk awania kuwa Mwanasoka Bora Ulaya 2019 dhidi ya Messi na Ronaldo

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

BEKI wa Liverpool, Virgil van Dijk atashindania taji la Mwanasoka Bora wa mwaka 2019 barani Ulaya baada ya kuorodheshwa katika wanafainali wa tatu wa mwisho katika kura zilizopigwa Agosti 15.

Mholanzi huyu atawania taji hilo la kifahari dhidi ya masupasta Lionel Messi (Barcelona) na Cristiano Ronaldo (Juventus), Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) limetangaza baada ya makocha 80 kutoka klabu zilizoshiriki mechi za makundi za Klabu Bingwa na Ligi ya Uropa na waandishi wa habari za michezo barani Ulaya kutoka mataifa 55 barani humo.

Mreno Ronaldo ni mshindi wa tuzo hii mwaka 2014, 2016 na 2017 naye raia wa Argentina Messi aliibuka mshindi mwaka 2011 na 2015.

Van Dijk anaingia katika orodha ya wawaniaji wa tuzo hii iliyoanzishwa mwaka 2011 kwa mara yake ya kwanza kabisa.

Mchango wake mkubwa katika safu ya ulinzi ya Liverpool ulisaidia timu hiyo kumaliza Ligi Kuu ya Uingereza katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City na kushinda Klabu Bingwa Ulaya na pia soka ya Uefa Super Cup iliyokutanisha wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya na Chelsea iliyonyakua Ligi ya Uropa.

Van Dijk, 28, aliibuka mwanasoka bora wa mwaka nchini Uingereza baada ya kung’ara msimu 2018-2019 na pia kutawazwa mchezaji bora wa msimu na wachezaji wanaosakata soka ya malipo nchini Uingereza (PFA).

Katika tuzo ya PFA alibwaga wachezaji Eden Hazard (Chelsea), Raheem Sterling, Sergio Aguero na Bernardo Silva (wote Manchester City) na mchezaji mwenza katika timu ya Liverpool, Sadio Mane.

Van Dijk aliibuka mchezaji bora wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya ambayo Liverpool ilicharaza Tottenham Hotspur 2-0 kupitia mabao ya Mohamed Salah na Divock Origi jijini Madrid nchini Uhispania mnamo Juni 1, 2019.

Mshambuliaji hodari Messi aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (LaLiga) na Bara Ulaya msimu 2018-2019 akishinda taji la 10 la Ligi Kuu nchini Uhispania.

Mvamizi matata Ronaldo alisaidia taifa lake kubeba taji la Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya (Uefa Nations League) na pia kuibuka mfungaji bora katika mashindano hayo pamoja na kufunga mabao mengi kuliko wote akiongoza Juventus kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Wachezaji walioorodheshwa katika mduara wa 10-bora, lakini wakachujwa baada ya raundi ya pili ya kura kwenye tuzo ya mwanasoka bora wa Bara Ulaya ni kipa Alisson Becker (Liverpool & Brazil), mshambuliaji Sadio Mane (Liverpool & Senegal), Mohamed Salah (Liverpool & Misri), Eden Hazard (Chelsea/Real Madrid & Ubelgiji), Matthijs de Ligt (Ajax/Juventus na Uholanzi), Frenkie de Jong (Ajax/Barcelona & Uholanzi) na Raheem Sterling (Manchester City & Uingereza).

Mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora barani Ulaya mwaka 2019 atafahamika Agosti 29 mjini Monaco. Uefa pia itatangaza droo ya mechi za makundi ya Klabu Bingwa ya msimu 2019-2020 siku hiyo.

Mbali na Ronaldo na Messi, washindi wengine wa tuzo hii ni Andres Iniesta (2012), Franck Ribery (2013) na Luka Modric (2018).

Orodha ya matuzo yatakayopeanwa Agosti 29:

Mwanasoka Bora wa msimu – Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Virgil van Dijk;

Kipa Bora wa msimu – Alisson Becker, Hugo Lloris, Marc-Andre ter Stegen;

Beki bora wa msimu – Trent Alexander-Arnold, Matthijs de Ligt, Virgil van Dijk,

Kiungo Bora wa msimu – Frenkie de Jong, Christian Eriksen, Jordan Henderson;

Mshambuliaji Bora wa msimu – Sadio Mane, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo;

Mwanasoka Bora wa mwaka wa kike – Lucy Bronze, Ada Hegerberg, Amandine Henry;

Mchezaji Bora wa msimu kwenye Ligi ya Uropa – Olivier Giroud, Eden Hazard, Luka Jovic