• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
‘Kufanya kazi katika boma la mwalimu ni baraka kwangu’

‘Kufanya kazi katika boma la mwalimu ni baraka kwangu’

Na MWANGI MUIRURI

KIJANA John Odhiambo, 19, alitua katika kijiji cha Kianda Kia Ambui ndani ya Kaunti ndogo ya Kigumo, Murang’a akisaka kazi ya kibarua Juni 2019 na akaipata katika boma la mwalimu mstaafu Bw Cyrus Ngugi.

Kazi yake huwa ni ya kuchunga ng’ombe, kulima na pia kuchota maji.

Ni kijana ambaye amewafurahisha wengi kutokana na hali yake ya roho safi na kupenda maisha yasiyo na presha.

Aidha, amejiheshimu kimaisha kiasi kwamba licha ya kuwa yeye ni kibarua anayefahamika tu kama ‘shambaboi’ hupenda hiyo kazi yake na pia hujipa kazi za ziada katika familia hii.

“Mshahara wangu ni wa Sh6,000 kwa mwezi. Chakula na nyumba ya malazi ni gharama ya mwajiri wangu. Mimi gharama zangu tu ni kutumia mshahara wangu,” aliambia Taifa Leo.

Pengine kosa lake kuu wakati wa mahojiano ni kuweka viatu mezani.

Kijana Odhiambo alianza kujipa jukumu la kupiga pasi nguo za Bw na Bi Ngugi na hapo akajipa hadhi ya kipekee katika maisha ya mwajiri wake ambaye humpa pesa za marupurupu akitekeleza majukumu hayo.

Kero ya Bw Odhiambo ni kuwa wenyeji katika kijiji hicho hawatilii maanani usafi wa mazingira na ndiyo maana ameanza kuonekana akifagia hata katika barabara inayoingia kwa mwajiri wake.

Kijana John Odhiambo, 19, ambaye ni mfanyakazi katika boma moja kijijni Kianda Kia Ambui, Kaunti ya Murang’a aking’arisha viatu vyake. Anapenda kazi yake na matumaini yake ni ya juu kuhusu kesho yake. Picha/ Mwangi Muiruri

Leo hii, wanakijiji wengi wameiga mfano wake na ambapo wameanza kutii ushawishi huu wa kuhakikisha udumishaji nidhamu na usafi wa kimazingara kijijini.

Bw Odhiambo mtakubaliana naye kwa mengi lakini kwa uchafu, kaa mbali naye.

Msikie anachokisema jirani yake mwalimu Ngugi.

“Nilikuwa ninafikiria huyu kijana ni wa familia ya huyu mwalimu. Nilishtuka kusikia kwamba yeye ni mfanyakazi. Huwa ni safi na huwezi ukaamini kuwa yeye ameajiriwa kazi ya shambani. Huyu ni kijana ambaye maisha yake hayana stresi hata kidogo,” anasema jirani wa familia hii ya Bw Ngugi.

Bw Ngugi anasema kuwa Bw Odhiambo huoga mwili kila siku na kwa bafu hukaa zaidi ya nusu saa akijing’arisha na kwa shughuli hiyo, kwa kila kuoga, lita 20 za maji hutumika.

Katika hali hiyo, amejishindia maisha ya u-celeb kwa kuwa jinsi ajitunzavyo ndivyo anajishindia hata ufuasi wa warembo katika eneo hilo.

Bw Odhiambo anasema hata ikiwa ni mfanyakazi wa shambani “siwezi nikawa na simu hivihivi.”

“Nimejinunulia simu ya Sh8,000 na silalamiki. Maisha ni kujipanga. Nguo siwezi vaa za mitumba na siwezi nikavaa viatu vya bei ya chini,” kijana huyu ajishasha.

Lengo

Anasema kuwa lengo kuu lake ni kufanya kazi kwa bidii katika familia hii, ajiwekee akiba ya kutosha ya kurejea kwao katika Kaunti ya Homa Bay akajenge nyumba na aoe msichana mrembo.

Hasa anasema anataka msichana wa kutoka jamii ya Agikuyu.

“Hawa warembo wa jamii hii hunichachawisha… Mimi sijui wamenipa nini na ni kama wamenilisha ndumba ya kimapenzi. Kuna wawili watatu jicho langu limewamulika na ninalenga kwamba wakati mwafaka ukiingia, nitamnyakua mmoja wao na nimfanye awe mke wangu,” anasema.

Lakini kabla ya kuoa au kujenga, analenga kujinunulia runinga moja kubwa, redio na hatimaye anunulie mrembo huyo anayelenga nguo za bei.

“Wewe bwana! Mimi sio wa bei rahisi. Pesa ndizo hunikosea. Lakini nazitafuta kwa njia halali na imani kwa Mola kuwa atanijalia ukwasi. Malengo yangu nitayatimiza na hata katika maisha ya usoni, utanipata nikiendesha gari la kifahari na nikiwa na watoto wanne safi na waliotunzwa… Wewe kaa hapo ukikosa kujiamini na una kazi unayolipwa mshahara wa mwisho wa mwezi,” akaambia mwandishi huyu.

Anasema kuwa hatawahi kujidharau, adharau kazi yake au adunishe pato lake.

“Nimekubali hali yangu kwa kuwa ni karo ya kusoma nilikosa. Lakini niko na kazi, makazi na kwa lishe sio gharama. Ikiwa hiyo tayari sio baraka, nionyeshe baraka ni gani,” anasema.

Kuhusu vile anatangamana na wenyeji ikifahamika kuwa kwa muda kumekuwa na kasumba ya uhasama wa kisiasa kati ya Wajaluo na Agikuyu?

“Hiyo ndiyo shida yenu waandishi wa habari… Unatafuta sasa kijisababu cha kunitenganisha na hawa watu wa kijiji hiki. Sisi sio wanasiasa na shida zetu zinafanana. Wanasiasa huko juu ndio hukosana. Sisi hapa ni ndugu na ikiwa unasubiri kuniona nikikorofishana na majirani, nafikiria utangoja kwa muda mrefu. Sisi wa kawaida hatuna chuki, chuki huchochewa na hao mlio nao huko kwa miji ya siasa,” anasema.

You can share this post!

Hamasisho la umuhimu wa noti mpya laendelea

Mwanga wa matumaini Sudan

adminleo