• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
ONYO LA THE REDS: Liverpool yawika Lampard akisifu ari ya Chelsea

ONYO LA THE REDS: Liverpool yawika Lampard akisifu ari ya Chelsea

Na MASHIRIKA

ISTANBUL, Uturuki

LIVERPOOL imetoa onyo kali kwa wapinzani wake barani Ulaya baada ya kutoka nyuma na kushinda Chelsea kwenye kandanda ya UEFA Super Cup kwa njia ya penalti mnamo Jumatano usiku.

Aidha, kocha Jurgen Klopp amemmiminia kipa Adrian sifa tele baada ya kupangua penalti iliyowezesha Liverpool kushinda Super Cup.

Adrian, ambaye alianzishwa mchumani kutokana na kipa nambari moja Allison Becker kuumia, alimzima Tammy Abraham na kuipa Liverpool ushindi wa penalti 5-4 baada ya mchuano huo unaokutanisha wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya na washindi wa Ligi ya Uropa kutamatika kwa mabao 2-2 katika muda wa ziada mjini Istanbul, Uturuki.

Adrian, 32, alijiunga na Liverpool bila ada ya uhamisho kutoka West Ham kujaza nafasi ya Simon Mignolet mnamo Agosti 5, siku moja baada ya vijana wa Klopp kupoteza dhidi ya Manchester City kwa njia ya penalti 5-4 kwenye soka ya Community Shield.

Kipa huyu wa zamani wa Real Betis alitupwa uwanjani kuchukua nafasi ya Alisson aliyeumia katika kipindi cha kwanza Liverpool ikichuana na Norwich katika mechi ya kufungua Ligi Kuu mnamo Ijumaa iliyopita. Liverpool ilitamba 4-1.

“Sijui Adrian alikuwa wapi wiki mbili zilizopita tukimenyana na Manchester City,” alisema Klopp baada ya kushuhudia vijana wake wakibeba Super Cup kwa mara ya nne.

“Nilipozungumza naye kwa mara ya kwanza, ilikuwa wazi atahitaji muda kuwa fiti, lakini hatukuwa na muda kwa hivyo lazima awe katika hali nzuri, na alikuwa hivyo; alicheza vizuri, alifanya maokozi muhimu.”

Adrian aondoa hatari

Adrian alidhihirisha yuko fiti aliporuka miguuni mwa Mateo Kovacic kuokoa hatari katika kipindi cha kwanza na pia kuondosha shuti la Mason Mount kabla ya dakika 120 kukamilika.

Pia alimchezea Abraham vibaya na kusababisha penalti katika dakika ya 101 iliyofungwa na Jorginho na kufanya mabao kuwa 2-2.

Bao la Sadio Mane dakika ya 95 lingeipa Liverpool ushindi katika muda wa ziada kabla ya penalti ya Jorginho kulazimisha mechi hiyo kuamuliwa kwa njia ya penalti.

“Kushinda kupitia penalti huwa ni bahati, lakini mchezo wake katika dakika 120 ulivutia sana. Kupangua penalti ya Abraham kulifanya ushindi huu uwe mtamu hata zaidi,” alisema Klopp.

“Alitusaidia sana na anastahili kujivunia kazi yake,” Mjerumani huyo alisema.

You can share this post!

Mwanga wa matumaini Sudan

Muumini apokonya kanisa viti

adminleo