SHERIA: Una haki kukataa mchumba wa kulazimishiwa
Na BENSON MATHEKA
WASOMAJI kadhaa wameniuliza iwapo inafaa wazazi kuwachagulia wanao wachumba.
Kulingana na Beatrice Kagwiria kutoka Marimanti, Tharaka Nithi, wazazi wake wanataka aolewe na mwana wa rafiki yao ambaye yuko ng’ambo.
Mwanadada huyu analalama kuwa wazazi wake wamemuonya asianzishe uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine wakisema wamekamilisha mipango ya ndoa na wazazi wa mchumba waliyemchagulia. Beatrice anahisi kwamba wazazi wake wanakiuka haki zake na anataka kujua ikiwa sheria inamkinga akikaidi wazazi wake.
Masaibu yake ni sawa na ya Nicholas Musyoka, barobaro wa miaka 23 kutoka Kileleshwa, Nairobi anayesema kwamba mama yake amemkataa mpenzi wake na kumchagulia kipusa kutoka kanisa analoabudu.
Msomaji huyu anasema kwamba mama yake anasema ni lazima aoe mwanadada wa tabaka lake naye anahisi kwamba mapenzi ni muhimu kuliko tabaka.
Anauliza ikiwa sheria inaruhusu wazazi kuchagulia wanao wao wachumba.
Wasomaji hawa wanawakilisha kadhaa ambao wamekuwa wakiniuliza swali hili.
Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, hakuna mtu anayefaa kulazimishwa kuolewa na au kuoa mtu asiyependa.
Sheria iko wazi kwamba ndoa ni kati ya mwanamume na mwanamke ambao wanakubali wao wenyewe kuoana bila kushinikizwa.
Hata wazazi wakichagulia mtu mchumba ni kinyume cha sheria kumlazimisha kuoa au kuolewa.
Sheria yakinga mtu
Ni kweli sheria inakinga mtu akikataa mchumba anayechaguliwa na mtu au watu wengine wakiwemo wazazi.
Hii ni kwa sababu haitakuwa hiari yao kuoa au kuolewa na mchumba waliyechaguliwa.
Kwa hakika muungano wowote usio wa hiari hautambuliwi kama ndoa.
Anayefungisha ndoa anafaa kuhakikisha sio ya kulazimishwa. Sheria ya ndoa haiweki mipaka ya matabaka, kabila au rangi.
Sheria inasema mradi mtu ametimiza umri wa miaka kumi na minane ana uhuru wa kuamua anayetaka kuoa au kuolewa naye.
Wanachofaa kufanya wazazi ni kuwashauri kuhusu masuala ya ndoa na kuwaachia wafanye uamuzi wao wenyewe.
Mtu ana haki ya kukataa mchumba asiye chaguo lake.