Makala

Kipi kitarajiwe baada ya BBI kukusanya maoni?

August 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya maridhiano (BBI) ilibuniwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM kutia saini muafaka uliotoa mapendekezo kadha yaliyolenga kuhakikisha uwepo wa umoja na utangamano nchini kuanzia uchaguzi mkuu ujao wa 2022.

Jopokazi hilo liliteuliwa na viongozi hao wawili na likatwikwa jukumu kuzunguka kote nchini kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa Wakenya kuhusu namna ya kusuluhisha changamoto kadhaa zinazochochea vita na mazingira hasi kila baada ya uchaguzi mkuu.

Masuala hayo ni ushindani au siasa za kikabila, ukosefu wa maadili ya kitaifa, kutokuwepo kwa ushirikishwaji wa wote serikali, kuhujumiwa kwa ugatuzi, utovu wa usalama, ufisadi, ukosefu wa haki katika chaguzi, kati ya mengine.

Sasa jopokazi hilo chini ya uenyekiti wa Seneta wa Garissa Yusuf Haji limekamilisha pilikapilika za kukusanya maoni, na mapendekezo kutoka kwa umma na sasa linatarajiwa kuandaa ripoti yenye mapendekezo kuhusu mabadiliko ya kisheria na kikatiba yanayopafaa kutekelezwa kushughulikia masuala hayo.

Mmoja wa makatibu wasaidizi wa jopo hilo la watu 14, wakili Paul Mwangi amethibitisha kuwa jopo hilo litakutana faraghani kuandaa ripoti yake itayowasilishwa kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga huku akifafanua kuwa ripoti hiyo itasheheni maoni ya Wakenya wote.

“Wakati huu (Alhamisi) tayari tumeanza mkutano wa kuandaa ripoti yetu. Tungependa kuwahakikisha Wakenya kwamba tutachambua maelezo, maoni, na mapendekezo yote ambayo tulipokea kutoka kwa wananchi katika vikao tulioandaa katika kaunti zote 47. Vilevile, tutashughulikia yaliyomo kwenye memoranda tulizopokea kutoka kwa makundi mbalimbali ya wadau,” akasema Bw Mwangi.

Alisema kuwa wanatarajia kukamilisha utayarishaji wa ripoti hiyo mwishoni mwa mwezi ujao wa Septemba.

Akiongea na wanahabari baada ya salamu za heri kati yake na Rais Kenyatta mnamo Machi 9, 2018, Bw Odinga alisema hivi:

“Tulipokutana na Rais, tulishiriki majadiliano ya kina. Tulitafakari kuhusu chanzo cha shida ambayo hukumba taifa hili kila baada ya uchaguzi. Kuanzia enzi ya hali ya hatari, majadiliano kuhusu uhuru na chaguzi za 1961 na 1963 na hatimaye wakati wa uhuru. Tulibaini kuwa taifa lilikuwa limeungana; watu hawakujichukulia kama wa kabila hili au lile. Baadaye tuligundua asili ya shida yetu. Vita baridi viligawanya wananchi lakini tuligundua kuwa tunaweza kuelekeza nchi katika mkondo wa utaifa. Tulitambua baadhi ya masuala ambayo yamekuwa yakisababisha migawanyiko nchini. Yalikuwa masuala tisa ambayo yalijenga mkataba wa maelewano kati yetu. Kisha tukateua jopokazi kuendelesha mipango ya kushughulikia masuala hayo kwa kushauriana na wananchi,” akasema Bw Odinga.

Hata hivyo, Bw Odinga na wanasiasa wanaounga mkono BBI, wanahisi kwamba kupanuliwa kwa kitengo cha utawala ndio suluhu la matatizo ambayo yamekuwa yakilizonga taifa hili kila baada ya uchaguzi mkuu.

Bw Odinga na chama chake cha ODM, wamekuwa wakiunga mkono mageuzi ya Katiba ili kuanzishwe mfumo wa utawala wa ubunge na kuondolewa kwa mfumo wa urais.

“Katika taifa lenye makabila mengi kama vile Kenya, mfumo wa utawala wa urais umeendeleza migawanyiko. Kila kabila huhisi salama ikiwa mtu wao yuko kileleni katika safu ya uongozi. Hii ndio maana kila baada ya uchaguzi, kabila wanakotoka wagombeaji wa urais walioshindwa huhisi kutengwa,” akasema Bw Odinga.

Hii ndio maana wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema huku BBI ikiendelea kuandika ripoti yake, Wakenya wasubiri kwa hamu mfumo wa utawala ambao itapendekeza kama suluhu la matatizo ambayo yamekuwa yakiisibu taifa hili kila baada ya uchaguzi wa urais.