• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
BBI 2: Huenda Uhuru na Raila wana njama fiche

BBI 2: Huenda Uhuru na Raila wana njama fiche

CHARLES WASONGA na VALENTINE OBARA

MASWALI yameibuka kuhusu nia halisi ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga baada ya kuamua kwamba Jopo la Maridhiano (BBI) liongezwe muda wa kuhudumu.

Maswali hayo ni kuhusu sababu ya kutaka ripoti nyingine na hali tayari walizindua nyingine mwezi uliopita.

Hii ni baada ya wawili hao kutangaza kuongezwa kwa muda wa jopo la BBI, hatua ambayo imepingwa na viongozi wa matabaka tofauti.

Kulingana na Bw Odinga, jopo hilo linatarajiwa kutoa ripoti mpya yenye marekebisho yatakayojumuisha, kuondoa au kuongeza masuala mengine ambayo hayamo kwenye ripoti ya kwanza.

“BBI imewezesha Wakenya kutoa maoni yao kuhusu masuala mazito yanayotishia taifa letu. Kuanzia sasa kuendelea mbele, kile tunachofaa kujadili ni kuhusu tunachohitajika kupitisha, kinachostahili kufanyiwa marekebisho, na kile ambacho kinatakikana kutupwa nje ya mapendekezo ya BBI ya kwanza,” akasema Bw Odinga baada ya kikao na wakuu wa chama chake cha ODM.

Kulingana na Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ripoti iliyozinduliwa ni “feki”: “Ripoti ya kwanza ilipendekeza kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka. Lakini kutokana na shinikizo kutoka kwa umma pendekezo hilo liliondolewa. Sasa wameongeza muda wa BBI ili itoe ripoti itakayolingana na matakwa yao,” akasema Bw Kuria.

Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, Kanisa la Kianglikana (ACK) kupitia kwa Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit, na Baraza Kuu la Kiislamu Nchini (Supkem) ni miongoni mwa waliopinga kuongezwa muda wa jopo hilo la watu 14 linaloongozwa na Seneta wa Garissa, Yusuf Haji.

Baadhi yao wanataka kuwe na jopo jipya la wataalamu wakisema hilo la BBI lina sura ya kisiasa.

ODM imekuwa ikipigania uwepo wa marekebisho katika mfumo wa ugatuzi ili kuwe na watawala wa maeneo ambayo zamani yalikuwa mikoa, kando na kuweka nafasi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa. Masuala haya hayamo kwenye ripoti ya kwanza ya BBI.

Wakati ilipozinduliwa, baadhi ya viongozi waliohutubu katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi wakiwemo Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli walisema ilistahili kupendekezwe nafasi ya waziri mkuu mwenye mamlaka.

Wabunge na maseneta za zamani kutoka Mlima Kenya pia wanataka wadhifa huo uwepo.

Wadadisi wa kisiasa wanaamini ukosefu wa pendekezo hilo ndio umemfanya Naibu Rais William Ruto na kikosi chake cha Tangatanga kubadili msimamo na kusema sasa wanaunga mkono BBI, ila ipitishwe ilivyo bila marekebisho.

Lakini katika hotuba yake jana, Bw Odinga alisisitiza kwamba yote wanayofanya na Rais Uhuru Kenyatta ni kwa maslahi ya taifa wala si kwa lengo la kufaidi watu kibinafsi.

Wiki iliyopita, wawili hao walikutana usiku na wanajopo wa BBI katika Ikulu ya Nairobi, kisha Ikulu ikatangaza jopo hilo limeongezwa muda wa kuhudumu ili lisimamie awamu itakayofuata ambayo inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu utekelezaji wa ripoti hiyo.

Haikujulikana ni kwa muda gani jopo hilo la BBI litaendelea kuhudumu lakini kulingana na ripoti yake, utekelezaji wake utafanywa ndani ya kipindi cha miezi 18.

You can share this post!

Mabasi ya Modern Coast yenye abiria 90 yanaswa Sultan Hamud

Kasisi motoni kwa kualika Tangatanga kwa harambee

adminleo