• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:03 PM
MWANASIASA NGANGARI: Mbiyu: Mwanasiasa aliyetuliza hasira za Mzee Jomo Kenyatta

MWANASIASA NGANGARI: Mbiyu: Mwanasiasa aliyetuliza hasira za Mzee Jomo Kenyatta

Na THE KENYA YEAR BOOK

PETER Mbiyu Koinange alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza kusomea katika Shule ya Upili ya Alliance mnamo 1926 na alikuwa Mkenya wa kwanza kutuzwa shahada ya Uzamili mnamo 1938.

Koinange alizaliwa mnamo 1907.

Baba yake, Chifu Mkuu Koinange wa Mbiyu, alimpeleka nchini Amerika mno 1927 kwenda kukamilisha elimu yake ya shule ya upili na kuendelea na elimu ya chuo kikuu.

Inasadikiwa kuwa Koinange alikuwa Mkenya wa kwanza kusomea nchini Amerika.

Koinange alikuwa msomi mtajika baada ya kupata elimu nchini Amerika na bara Ulaya.

Baadaye alitokea kuwa mwandani wa Rais wa Kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta. Uhusiano wake wa karibu na Mzee Kenyatta ulifanya wandani wake kumpachika jina la majazi la Kissinger (jina la Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Henry Kissinger).

Alisomea katika chuo cha Hampton jimboni Virginia Magharibi na kisho akajiunga na Chuo Kikuu cha Ohio Wesleyan ambapo alihitimu kiwango cha digrii.

Baadaye alisomea digrii ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Aliporejea humu nchini, yeye na baba yake walianzisha Chuo cha Ualimu cha Githunguri, Kiambu ambacho baadaye kiligeuka kuwa kitovu cha makabiliano dhidi ya utawala wa wakoloni.

Kati ya 1938 na 1947, Koinange alikuwa mkuu wa Chuo cha Ualimu cha Githunguri, na mwakilishi wa chama cha Kenya African Union (KAU) barani Ulaya kati ya 1951 na 1959.

Mnamo 1947, Koinange alimkabidhi Mzee Kenyatta chuo cha ualimu na kuelekea Uingereza kusomea diploma katika Chuo Kikuu cha London.

Baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Uchumi cha London kusomea uzamili.

Koinange aliishi Uingereza kwa miaka mingi wakati ambapo vita vya Mau Mau vilikuwa vimeshika kasi nchini.

Akiwa Uingereza, Koinange alijiunga na Waafrika wengine kufanya maandamano dhidi ya utawala wa wakoloni.

Hapo ndipo alikutana na mwasisi wa Ghana Kwame Nkrumah na nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilipopata uhuru hatimaye mnamo 1957, Nkrumah alimpa Koinange kazi ya mkurugenzi wa Idara ya Kushughulikia masuala ya Afrika mjini kati ya 1959 na 1961.

Jijini London, Koinange pia alikutana na wanaharakati wa kupigania ukombozi wa Afrika kama vile Nnamdi Azikiwe wa Nigeria, George Padmore wa Trinidad na Fenner Brockway, Mwingereza ambaye –alikuwa mwanaharakati wa kukemea dhuluma zilizotekelezwa na wakoloni.

Stakabadhi za siri zilizotolewa hivi karibuni na kikosi cha Usalama cha Uingereza, maarufu M15, zinaonyesha kuwa Chifu Mbiyu alipokea barua tele kutoka kwa marafiki wa Koinange.

Stakabadhi za siri zilizotolewa hivi karibuni na kikosi cha Usalama cha Uingereza, maarufu M15, zinaonyesha kuwa Chifu Mbiyu alipokea barua tele kutoka kwa marafiki wa Koinange wa humu nchini na kote duniani.

Barua hizo zilitoka kwa makundi mbalimbali kama vile Chama cha Marafiki Duniani, Chama cha Wahudumu wa Teksi nchini, Chama cha Maskwota na Wamiliki wa Mashamba, Chama cha Kitaifa cha Jamii ya Wasomali, Chama cha Vijana Zanzibar, Chama cha Wafanyakazi katika Sekta ya Petroli nchini Japan, na kadhalika.

Oginga Odinga alimwalika Koinange kuhudhuria kongamano la Lancaster, Uingereza, kuhusu katiba mnamo 1960.

Mwaka uliofuatia Koinange alirejea nchini Kenya kutoka Uingereza na akachaguliwa kuwa mbunge wa Kiambaa mnamo 1963 ambapo Rais Kenyatta alimteua kuwa waziri wa Masula ya Ukombozi wa Afrika.

Alihudumu kwa muda mfupi na kisha akahamishiwa katika afisi ya rais ambapo aliteuliwa kuwa waziri wa Utawala wa Mikoa mnamo 1966. Alihudumu katika wadhifa huo hadi 1978 ambapo Mzee Kenyatta alifariki.

Aliporejea kutoka Uingereza wengi walidhani kwamba Koinange angetwaa uongozi wa chama cha Kanu. Lakini alikataa akisema kuwa Mzee Kenyatta alikuwa na sifa bora za uongozi.

Koinange na Kenyatta walikuwa marafiki wa dhati na waliitana jina la utani: Ngorobi (yaani mgomvi).

Wengi wamekuwa wakisema kuwa Koinange ndiye alikuwa akiendesha serikali.

Kila mara Mzee Kenyatta alipokasirika, Koinange na Mkewe Rais Mama Ngina Kenyatta ndio waliweza kumfikia na ‘kumpoza’.

Lakini Mkuu wa Watumishi wa Umma wa pili katika utawala wa Kenyatta, Geoffrey Kareithi, amekanusha madai kwamba Koinange alikuwa akiendesha serikali.

Kareithi, hata hivyo, anakiri kwamba Kenyatta na Koinange walikuwa marafiki wa dhati.

Anasema kuwa kuna wakati Kenyatta alimtaka Koinange kutoka nje alipokutana na baadhi ya maafisa serikalini.

Kenyatta na Koinange walikutana kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mnamo 1936.

Koinange alisoma katika chuo cha Cambridge, kupitia ufadhili wa Canon Leakey, babu yake mwanaharakati wa mazingira humu nchini Richard Leakey. Naye Kenyatta alikuwa jijini London akiwa mwanafunzi na mwakilishi wa chama cha Kikuyu Central Association (KCA).

Koinange alikiri kuwa mafanikio yake katika siasa yalitokana na uhusiano wake wa karibu na Mzee Kenyatta.

Wengi walidhani kuwa Koinange alikuwa miongoni mwa watu wa karibu wa Mzee Kenyatta ambao hawakutaka Makamu wa Rais Daniel Moi kuchukua mamlaka baada ya kifo cha Mzee mnamo 1978. Lakini yeye hakuwa miongoni mwa waliotaka kumzuia Moi.

Koinange aliandamana na Kenyatta kila mara alipoenda; katika Ikulu ya Nairobi, Mombasa au Nakuru na alikutana na familia yake mara chache sana.

Familia ya Koinange ilifuatilia vyombo vya habari ili kujua mahali ambapo Kenyatta angezuru ili waende huko kukutana na baba yao. Katibu wa Koinange, Carmen Pereira ndiye alijitwika jukumu la kuhudhuria harusi za kifamilia, kulipa karo ya watoto, kujibu barua za kibinafsi na hata kupokea wageni.

Stakabadhi za kulipa karo za watoto wake na barua za kibinafsi zilichanganyikana na stakabadhi za serikali katika kabati lake ofisini.

Kuthibitisha hili, ni barua iliyoandikwa mnamo Juni 1970 iliyopatikana kabatini baada yake kuondoka serikalini. Barua hiyo ilifichua kuwa Koinange alikuwa mwanachama wa kundi la Freemason.

Kutokana na shughuli nyingi, Koinange alimteua kaka yake, Charles Karuga, kuendesha shughuli zote kwa niaba yake.

Nduguye alimfanyia shughuli nyingi, yakiwemo masuala ya ardhi.

Lakini familia yake inasema kuwa Koinange hakutumia urafiki wake na Mzee Kenyatta kujitajirisha.

Koinange alipoaga dunia hakuwa na mali. Baada ya kifo chake familia yake ilibaini kwamba Koinange aliacha Sh12,000 tu katika benki moja jijini London.

Kadhalika, aliiachia familia yake mzigo wa madeni.

Ndugu yake Karuga alikopa hela kumnunulia mashamba Koinange kutokana na hofu kwamba angekufa akiwa maskini licha ya kuwa na ushawishi mkubwa serikalini.

Inadaiwa kuwa Karuga wakati mmoja alimsihi Kenyatta kuhakikisha kwamba Koinange anapata kitu ambacho watoto wake wangerithi.

Wakati mwingine, Koinange pia alijionyesha kwamba alikuwa na ushawishi serikalini.

Mnamo 1975, alikataa kufika mbele ya jopo lililokuwa likichunguza kifo cha aliyekuwa mbunge wa Nyandarua, J.M. Kariuki.

Jopo hilo lilikuwa likiongozwa na Elijah Mwangale, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa waziri katika serikali ya Moi.

Makamu wa Rais Moi na aliyekuwa Mkuu wa Sheria Njonjo walifika mbele ya jopo hilo kutoa ushahidi wao.

Koinange alikataa kusema ikiwa alipokea barua iliyomtaka kufika mbele ya jopo hilo au la.

Miaka mingi baadaye, mmoja wa wake zake, aliambia wanahabari kuwa Koinange alikataa kufika mbele ya jopo hilo kwa sababu watu tayari walikuwa wanaamini kwamba alihusika na kifo cha JM Kariuki.

Mkewe pia alisema Koinange alikataa kuomba radhi kwa jopo hilo kwa sababu wangedhani kwamba anawaogopa.

Ripoti ya uchunguzi ilipokabidhiwa kwa Kenyatta, rais aliagiza jopokazi hilo kuihariri na kuondoa jina la Koinange.

Kenyatta alisema kuwa kumhusisha Koinange na mauaji kulimaanisha kwamba walimrejelea yeye.

Mwenyekiti wa jopokazi hilo aliondoa jina la Koinange kwenye ripoti.

Mnamo Agosti, 1978, Koinange alikuwa na Kenyatta jijini Mombasa. Lakini baadaye aliomba apewe ruhusa ya siku moja huku akiahidi kwamba angerejea baada ya siku moja.

Kenyatta alifariki usiku kabla ya Koinange kurejea.

Koinange alfajiri alifahamishwa na Kamishna wa Mkoa wa Pwani Eliud Mahihu kwamba Kenyatta aliaga dunia.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa ushawishi wa Koinange.

Kulingana na waliomfahamu, Koinange alionekana dhaifu na kupoteza matumaini na alifariki dunia mnamo Septemba 1981, miaka mitatu baada ya kifo cha Kenyatta. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 74.

You can share this post!

Raila, Mudavadi watofautiana kuhusu kura ya maamuzi

DINI: Utakifanyaje kifo chako kuwa zawadi kwa wengi ili...

adminleo