DINI: Utakifanyaje kifo chako kuwa zawadi kwa wengi ili uombolezwe kwa heshima?
Na FAUSTIN KAMUGISHA
KIFO ni mtihani.
Kuna aliyesema dunia ni mahali pa hatari sana, hutoki ukiwa hai.
Hadithi inapokuwa nzuri kwenye gazeti hukatizwa na kuandikwa itaendelea toleo lijalo.
Mtu anapoaga dunia ni Mungu hukatiza hadithi ya maisha yake na kuandika kuwa itaendelea toleo lijalo.
Swali linabaki nani ataomboleza utakapoaga dunia?
Tunaalikwa kuwalilia walioaga dunia.
“Mwanangu, mlilie mtu aliyekufa;lia kwa uchungu, kuonesha huzuni yako. Uuzike mwili wake kwa heshima ipasavyo, wala usipuuze mazishi yake. Lia kwa uchungu na kwa moyo, hudhuria matanga kama anavyostahili marehemu, omboleza siku mbili tatu usije ukasemwa; kisha ufarijike kutokana na huzuni yako” (Yoshua Bin Sira 38:16-17).
Bila shaka marehemu anakuwa kwenye moyo wako, sababu alikugusa.
Kuna methali ya Ujerumani isemayo, hastahili kuishi anayeishi kwa ajili yake tu. Ukiwafia wengine, unakifanya kifo kiwe zawadi kwa wengine. Kwa namna hiyo utakapoaga dunia watu wengi wataomboleza. Kuomboleza kunahusishwa na kukuombea na kukupendekeza kwa Mungu.
“Ni baraka kufia jambo fulani, sababu unaweza kwa urahisi kufa bure,” alisema Andrew Young. Kuwafia wengine hakuhitaji kujipendelea. Mtu anayejipendelea hafikirii kama kuna wengine duniani anajiona kitinda mimba duniani.
Kuna hadithi juu ya mtu aliyekuwa kwenye kitanda cha mauti. Aliwaambia waliomzunguka: “Nilifia masomo ya kidato cha nne nikashinda mtihani. Nilifia masomo ya kidato cha sita, nikashinda mtihani. Nilifia masomo ya chuo kikuu, nikashinda. Nilipooa, niliifia familia. Baadaye niliwafia watoto, wapate maisha mazuri. Nilifia mambo mengi kama kusemwa vizuri, kuwapendeza watu lakini nilisahau kuishi.” Ndugu msomaji unafia nini? Usisahau kuishi.
Ukiacha umeandika wosia, kifo chako kinakuwa zawadi na si sababu ya malumbano. Ukiwaachia urithi wa elimu watoto wako kifo chako kinakuwa zawadi. Juu ya kufanya vifo vyetu viwe zawadi, Henri J.M.Nouwen mwandishi wa vitabu alikuwa na haya ya kusema, “Namna gani tunafanya vifo vyetu zawadi kwa wengine?
Mara nyingi maisha ya watu yanaharibiwa, yanadhuriwa au kuwa na majeraha maisha yao yote kwa vifo vya jamaa au marafiki zao. Lazima tufanye tuwezalo ili kukwepa hili.Tunapokuwa karibu kifariki, tunalowaambia wale ambao wako karibu nasi, iwe kwa kusema au kuandika ni muhimu. Tunapowashukuru, kuwaomba msamaha kwa makosa yetu na kuwasamehe na kuwaonesha nia ya kutaka waendelee na maisha yao bila kusutwa lakini wakikumbuka neema za maisha yetu, basi vifo vyetu vinakuwa zawadi kweli.”
Hasara kubwa si kifo bali kinachokufa ndani yetu. “Kifo si hasara kubwa sana katika maisha yetu. Hasara kubwa sana ni kile kinachokufa ndani yetu wakati tunaishi,” alisema Normani Cousins mtunga insha na mwariri wa Amerika (1912 – 1990). Wakati tunaishi kuna mambo ambayo yanaweza kufa kama shauku, moyo wa kutoa, moyo wa kujitolea, uchaji kwa Mungu, utii, usafi wa moyo. Vikifa ni hasara kubwa.
“Jambo baya sana maishani si kwamba tunakufa, bali kile kinachokufa ndani ya mtu wakati anaishi,” alisema Albert Schweitzer.
Jambo baya sana ni matumaini kufa wakati unaishi, utu kufa wakati unaishi, ukarimu kufa wakati unaishi, moyo wa kutendea wengine mema wakati unaishi, mtazamo chanya kufa wakati unaishi na moyo wa kazi kufa wakati unaishi. Huku ni kufa mara mbili kama mkaa. Mara ya kwanza ni tunu na fadhila moyoni mwako kufa. Na mara ya pili ni kuaga dunia. Hayo yakishasemwa kifo kinabaki kuwa mtihani. Takwimu kuhusu kifo ni za kutisha. Kati ya watu elfu moja, elfu moja wote wataaga dunia. Kifo ni mtihani. Mtoto anapozaliwa analia, watu wanafurahi. Mtu anapokufa watu wanalia.
“Kuaga kwangu dunia kutakuwaje? Sote tutaonja kuzama kwa jua! Je jambo hilo tunalitazamia kwa matumaini? Tunalitazamia na furaha ile ya kukaribishwa na Bwana?” alisema Papa Francis.
Kwake papa na ilivyo kwa waumini wa dini mbalimbali, kuna maisha baada ya maisha.