Wapwani wakae ange upepo mkali ukitarajiwa wiki hii
NA MWANDISHI WETU
IDARA ya Utabiri wa hali ya Hewa imewaonya wakazi wa Pwani na Mashariki kwamba upepo mkali unaosababisha maafa unatarajiwa maeneo hayo wiki hii.
Kaunti ambazo wakazi wake wametakiwa kutahadhari kutokana na upepo huo ni Tana River, Lamu, Kilifi, Mombasa, Kwale na Taita Taveta.
“Upepo mkali ambao unavuma kwa mita 12.5 kwa sekunde unatarajiwa upande wa Mashariki mwa nchi. Upepo huo pia utavuma kwenye Bahari Hindi na kuathiri maeneo ya Pwani,” akasema Mkurugenzi wa idara hiyo, Stella Aura.
Tangazo hilo ni sawa na lile lililotolewa na Mamlaka ya Usafiri Majini (KMA) mnamo Alhamisi wiki iliyopita kwamba upepo mkali unaovuma kwa mita 20 kwa kila sekunde utashuhudiwa Pwani na Mashariki kwa siku tatu mfululizo.
“Wasafiri wa majini na wenyeji wa maeneo yaliyotajwa wanatakiwa kujihakikishia usalama wao,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa KMA, Meja Mstaafu George Okong’o.
Idara hiyo pia ilitangaza kuwa mvua kubwa itanyesha katika kaunti za Ziwa Viktoria na Bonde la Ufa huku eneo la Nairobi na eneo la Mlima Kenya zikishuhudia baridi kali na mawingu mengi angani.
Kaunti zitakazopokea mvua ni Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Laikipia, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia. Kando na jiji la Nairobi hali ya baridi kali na mawingu mengi yaliyotanda angani itashuhudiwa katika kaunti za Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka-Nithi.