Kimataifa

Bomu lalipuka na kuua watu 63 harusini

August 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA AFP

WIZARA ya Usalama wa Ndani nchini Afghanistan imethibitisha kwamba watu 63 wameaga dunia kutokana na kisa cha kulipuliwa kwa bomu na mlipuaji wa kujitolea mhanga wakati wa sherehe za harusi kwenye ukumbi mmoja mjini Kabul mnamo Jumamosi.

Msemaji wa wizara hiyo Nasrat Rahimi alisema kwamba idadi ya majeruhi ilikuwa imefikia watu 182 huku wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo ya wanandoa wawili kufunga pingu za maisha.

Kulizuka patashika kwenye ukumbi huo huku moshi ukitanda na matone ya damu yakitapakaa kila mahali kila aliyehudhuria akikimbilia usalama wake wakati wa mlipuko huo wa ghafla usiotarajiwa kutokea.

Hata hivyo, kundi la kigaidi la Taliban ambalo lilidaiwa kuhusika na tukio limekanusha na kusema kwamba limekuwa likiheshimu makubaliano kati yao na Marekani kuhusu kupunguzwa kwa wanajeshi wake nchini Afghanistan. Kulingana na makubaliano hayo, Taliban iliaahidi kutoendeleza ugaidi huku Marekani ikipanga kuwaondoa majeshi yake ambayo yamekuwa yakishika doria kwa miaka kadhaa nchini humo.

Kulingana na mashahidi, zaidi ya watu 1,200 walikuwa wamehudhuria sherehe hiyo. Miili ya watu walioaga dunia na waliojeruhiwa bado ilikuwa ikitolewa kwenye ukumbi huo wa sherehe saa mbili baada ya tukio hilo.

Harusi hiyo iliaminika kuwa ya Waislamu wanaoegemea dhehebu la Shia ambao mara nyingi hulengwa na wenzao wa kundi la Sunni ambao ndio wengi zaidi Afghanistan.

Harusi nchini Afghanistan huwa zimejaa mahanjam na shamrashamra nyingi na maelfu ya wageni huhudhuria. Wakati wa harusi wanaume huketi eneo tofauti na watoto na wanawake.

Kulingana na Mohammed Farhag ambaye alikuwa kwenye harusi hiyo, alikuwa kwenye eneo wanakoketi wanawake aliposikia mlipuko upande wa wanaume.

“Nilikimbia nikilia na kuelekea nje. Kwa zaidi ya dakika 20, ukumbi ulikuwa umejaa moshi. Karibu kila mtu aliyekuwa upande wa wanaume amefariki au kupata majeraha mabaya,” akasema Bw Farhag.

Magaidi wamekuwa wakitekeleza mashambulizi kwenye harusi zinazofanyika Afghanistan kwa sababu mikakati tosha ya usalama huwa haipo.

Mnamo Julai 12, zaidi ya watu sita waliaga dunia wakati mlipuaji wa kujitolea mhanga alivamia harusi iliyokuwa ikiendelea katika mkoa wa Nangarhar. Kundi la kigaidi la IS ambalo limekuwa likiendeleza mauaji mkoani humo lilikiri kuhusika na shambulizi hilo.