• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
Raha kijijini baada ya baba kumuua mwanawe!

Raha kijijini baada ya baba kumuua mwanawe!

NA SHABAN MAKOKHA

JAPO kifo huandamana na machungu, wakazi wa kijiji cha Eshirembe, eneobunge la Butere, Kaunti ya Kakamega wameshangaza ulimwengu kwa kusherehekea mauti ya mwanaume aliyekatwa kwa panga na babake Jumapili jioni kwa kuiba mahindi kisha kuyauza

Mzee John Makokha, 78 alimuua mwanawe Habil Amunza kwa kumkata kwa panga kwa kutenda kosa hilo huku wanakijiji nao wakifurahi na kumsifia kwa kuwaokoa dhidi ya maovu ya mwendazake.

Wakazi walimtaja Bw Amunza kama mwizi sugu ambaye amebobea katika kuwapokonya watu wengine mali yao, wakidai amewaua na kuwajeruhi baadhi ya wanakijiji miaka ya nyuma.

“Baba na mwanawe wamekuwa wakigombana kila mara na tulikuwa na hofu kwamba Bw Amunza angemgeukia mzazi wake na kumuua jinsi ambavyo amekuwa akiwaua wanakijiji. Kwa bahati nzuri ni babake aliyemuua. Mungu ni mkuu,” akasema Mzee Jared Nandwa, 82.

Juhudi za kumfikia Naibu Kamishina wa Kaunti ndogo ya Butere Achoka Julius kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba baada ya kukosa kupokea simu au kujibu jumbe ambazo Taifa Leo ilimtumia.

Mkewe Mzee Makokha alifariki mnamo Januari mwaka huu na kumwacha na kijana huyo msumbufu aliyeogopwa na kila mwanakijiji.

Mzee Nandwa ambaye ni jirani ya familia hiyo alisimulia kwa machungu namna mwendazake alimuua mwanawe wa kiume Edwin Alubokha miaka tisa iliyopita.

“Alikuwa rika moja na mwanangu wa kiume na walikuwa wakicheza pamoja kila mara. Hata hivyo, Bw Amunza alikumbatia maisha mabaya ambayo yalihuzunisha sana wanakijiji. Alimpiga mwanangu, Bw Alubokha kichwani akitumia kiti na mtoto wangu akafa papo hapo. Alikamatwa kisha akaachiliwa miezi minne baadaye katika hali ya kutatanisha,” akasema Mzee Nandwa.

Mkongwe huyo alisimulia jinsi sherehe za kuadhimisha maisha ya mkewe Mzee Makokha zilivyonoga kwenye boma hilo mnamo Jumamosi lakini hali ikageuka baada ya marehemu kuiba mahindi siku iliyofuatia. Tabia hiyo ilimghadhabisha babake ambaye alimkata kwa panga alipokanusha kuitekeleza.

Chifu wa Lokesheni ndogo ya Eshirembe Aggrey Maina alisema alijuzwa kuhusu kifo hicho jana ndipo akafika nyumbani kwa marehemu.

“Nilipata mwili wa marehemu ukilowa damu kwenye mlango wa nyumba yake. Niliwaita polisi ambao waliusafirisha hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kakamega,” akasema afisa huyo wa utawala.

You can share this post!

Magoha adinda kutetea wanavyuo wanaokosa hafla

Maraga akiri majaji wamezembea kuamua kesi

adminleo