• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Kenya yafundishwa magongo

Kenya yafundishwa magongo

JOHN KIMWERE Na GEOFFREY ANENE

KENYA imejifunza mambo kadhaa baada ya kupokezwa vichapo kwenye mechi za magongo ya wanaume na wanawake za kuwania tiketi ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki mwaka 2020 zilizochezewa Uwanja wa Chuo Kikuu cha Stellenbosch mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Baada ya kupoteza mechi nne za kwanza, Chui ilikuwa katika hatari ya kuvuta mkia bila alama ikiteremka uwanjani Stellenbosch kuzichapa dhidi ya Namibia.

Hata hivyo, ilianza vyema mchuano huu, ingawa ilijipata ikishambuliwa vikali zaidi baada ya kufungua ukurasa wa magoli katika kipindi cha pili. Mabao mawili ya haraka katika dakika 15 za mwisho, moja kutoka kwa Constant Wakhura, yaliimarisha uongozi wa Chui hadi 3-0 kabla ya Namibia kupata bao la kujiliwaza.

Ushindi huu ulihakikisha Kenya inamaliza kampeni yake kwa kuruka Namibia kwenye jedwali la mashindano haya ya mataifa sita.

Afrika Kusini na Misri, ambazo zilishinda mechi zao nne za kwanza, zitakutana katika fainali ya kufa-kupona baadaye Agosti 18 kuamua nani kati yao ataingia Olimpiki mwaka 2020.

Ghana ni ya tatu kwa alama sita baada ya kulemea Zimbabwe 4-3 katika mechi yake ya mwisho Jumapili. Zimbabwe imekamilisha katika nafasi ya nne kwa alama nne, alama moja mbele ya Kenya. Namibia imemaliza mkiani kwa alama moja.

Timu ya taifa ya wanawake maarufu ‘Tausi’ chini ya kocha, Tom Olal iliteleza na kuibuka ya nne kwa alama nne baada ya kushinda mechi moja, kutoka nguvu sawa mara moja na kudondosha patashika tatu. Hata hivyo, timu ya wanaume ilijikuta njia panda ambapo ilimaliza ya tano kwa alama tatu baada ya kushinda mechi moja na kuyeyusha patashika nne.

Timu za Afrika Kusini (wanaume na wanawake) ziliendeleza ubabe wazo na kutwaa tiketi ya kushiriki Olimpiki za Tokyo mwaka 2020. Matokeo ya kenya yaligadhabisha wengi akiwamo Dennis Owoka kocha wa Butali Warriors ambayo ndiyo wafalme wa mchezo huo nchini.

”Wanamagongo wa Kenya wanahitaji kuwa wakikaza safu ya difensi ili kuwapiga breki wapinzani wao,” anasema na kuongeza kuwa pia wanastahili kushirikiana vyema Uwanjani ili kufanya rahisi kwao kutengeneza nafasi za kufunga.

Matokeo ya Kenya yalikuwa hivi kwa wanawake:Namibia 0-1 Kenya, Ghana 1-1 Kenya, Kenya 0-2 Zimbabwe, Afrika Kusini 3-0 Kenya.

Wanaume: Ghana 3-2 Kenya, Misri 7-2 Kenya, Kenya 2-3 Zimbabwe, Afrika Kusini 4-0 Kenya na Kenya 3-1 Namibia. 

You can share this post!

Chapa Dimba Season Three kuanza Septemba

Olunga afungia Kashiwa Reysol bao la ushindi

adminleo