Raila na Kalonzo ni wasaliti – Mudavadi
Na DERICK LUVEGA na JUSTUS OCHIENG’
KIONGOZI wa Chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi amewakashifu viongozi wa upinzani wanaoshirikiana na serikali akiwataja kama wanafiki wasiokuwa na msimamo wowote wa kisiasa.
Bw Mudavadi ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali baada ya kinara wa ODM Raila Odinga kuridhiana na Rais Uhuru Kenyatta, alitangaza kuwa hatafuti kazi serikalini kama viongozi wenzake katika Muungano wa NASA.
“Ni unafiki kwa baadhi ya viongozi kushirikiana na serikali ilhali wanadai bado wako kwenye upinzani. Huwezi kamwe kuwa serikalini na upinzani kwa wakati moja,” akasema Mudavadi akiwa katika Kaunti ya Vihiga.
Hata hivyo, mwanasiasa huyo alisema bado anasubiri mapendekezo ya kamati ya maridhiano (BBI) iliyobuniwa na Rais na Bw Odinga japo akafichua kwamba iwapo kura ya maoni itaandaliwa nchini, basi isizingatie hoja ya kubuni vyeo kwa ‘watu fulani’ lakini izingatie maslahi ya Wakenya.
Makamu huyo wa zamani wa Rais alibainisha wazi kuwa hatafuti kazi serikalini akiahidi kwamba ataunda utawala wake baada ya kutwaa ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
“Nimesema mara kadhaa kwamba sitaki kazi ya serikali. Mimi niko upinzani na sitakubali kupewa kazi katika serikali ya sasa. Nasubiri mwaka wa 2022 kuunda serikali yangu,” akasisitiza Bw Mudavadi.
Aheshimu uamuzi wa wapigakura
Kigogo huyo wa siasa za Magharibi alisema anaheshimu uamuzi wa raia ndiyo maana alipobwagwa kwenye uchaguzi wa ubunge wa Sabatia mwaka wa 2002 kwa kuunga mkono azma ya Rais Kenyatta kuingia mamlakani, alisalimu amri na kuwa nje ya siasa kwa muda wa miaka mitano.
Aidha alisema wafuasi wa NASA wameshangazwa na hatua ya viongozi wao kuingia kwenye ‘ndoa’ na serikali ya Jubilee ilhali muungano huo haujatimiza malengo ya kubuniwa kwake.
“Mimi ndiye niliunda muungano wa Nasa. Tulishinda uchaguzi lakini tukaibiwa kura. Wafuasi wetu sasa wanatuangalia na kushangaa iwapo kwa kweli tunaheshimu malengo tuliyokusudia kutimiza kwa taifa hili,” akaongeza Bw Mudavadi.