• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
GWIJI WA WIKI: Salyne Nyongesa

GWIJI WA WIKI: Salyne Nyongesa

Na CHRIS ADUNGO

MSHUKURU sana Mwenyezi Mungu kwa neema ya afya aliyokujalia.

Mshukuru kila siku kwa uzima na uhai na umwombe akupe nguvu zaidi ya kumtumikia.

Mola akikutunukia yote haya, pania sana kutumia kila fursa uipatayo kufanya mambo yatakayomfurahisha na kuridhisha nafsi za binadamu wenzako.

Usibabaishwe na shetani kwa kuwa yupo siku zote kukutia majaribuni. Badala ya kupotezewa dira na changamoto, jibidiishe maradufu ili ufanikiwe na ujiwekee viwango vipya vya malengo ya mara kwa mara.

Ukifanya hivyo na kuwaheshimu wadogo kwa wakubwa wako, bila shaka nyota yako itang’aa. Itametameta na kuangaza mbali. Matokeo yatakuwa ni milango yako ya heri kujifungua yenyewe.

Hii ndiyo nasaha ya Bi Salyne Nyongesa – mwandishi mahiri na mpenzi kindakindaki wa Kiswahili ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Immaculate Girls, Kitale.

Maisha ya awali

Salyne alizaliwa mnamo 1977 katika kijiji cha Tabani, kata ya Kiminini, Kaunti ya Trans-Nzoia. Wazazi wake ni Mzee Justus Nyongesa na mama Mary ‘Khakoni’ Naliaka.

Alianza safari yake ya masomo katika Shule ya Msingi ya Tabani. Alama nzuri alizozipata katika mtihani wa kitaifa mnamo 1990 zilimpa fursa ya kujiunga na Shule ya Upili ya Lugulu Girls alikosomea kati ya 1991 na 1994.

Mnamo 1996, alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Mwalimu wake wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Tabani, Bw James ndiye alimwekea msingi imara wa kupenda na kukichangamkia Kiswahili alaa kulihali.

“Kila alipoingia darasani kufundisha, Bw James alikuwa na mazoea ya kutaja majina ya wale wanafunzi ambao kulingana naye, hawakuwa na sababu ya kukosa alama ya ‘A’ katika mtihani wao wa kitaifa. Ajabu ni kwamba kila wakati jina langu ndilo lililokuwa la kwanza katika orodha yake. Alinifanya kuhisi kwamba nina uwezo wa kufaulu,” anasema Salyne.

Ni kutokana na motisha hii ya mwalimu wake ambapo alijipata akijitahidi masomoni huku akijijengea desturi ya kusoma vitabu vingi vya hadithi za Kiswahili.

Alipojiunga na shule ya upili, anakiri kwamba aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Lugulu Girls wakati huo, Bi Priscillah Were ndiye alimwelekeza vilivyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Alimhimiza kuwa na msimamo imara na kudumisha uhai wa ndoto zake za siku za halafu. Ni Bi Were ndiye alimfanya kuvutiwa sana na taaluma ya ualimu hasa baada ya kumtanguliza vyema katika somo la Fasihi ya Kiswahili.

“Alizoea sana kuuliza maswali darasani na kuniteua mara kwa mara kuyajibu. Wepesi wangu wa kujieleza kwa ufasaha mkubwa ni kiini cha Bi Were kunipa majukumu ya kuwa mwelekezi wa midahalo na vipindi vyote vya mijadala. Alianza kuniita mwalimu wakati ningali mwanafunzi,” asema Salyne kwa kusisitiza kuwa hajutii kabisa kuwahi kujitosa katika ulingo wa ukufunzi.

Salyne kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Laikipia chini ya uelekezi na usimamizi wa Dkt Sheila Wandera-Simwa.

Ingawa anajivunia mafanikio mengi, anakiri kuwa safari yake ya maisha ya awali ilikuwa ngumu na yenye panda-shuka tele.

“Kipindi chote nikiwa mwanafunzi, niliishi katika

mazingira mabovu yaliyonihini fursa ya kujivunia vitu vingi vya kimsingi. Nakumbuka nilikosa karo nikiwa mwanafunzi wa shule ya upili na chuo kikuu. Hali hiyo iliniweka katika ulazima wa kusitisha masomo kwa muda, nikarejea nyumbani kwa siku, wiki na miezi.”

Hata hivyo, changamoto hizo zilimkomaza na kumpa sababu tosha za kutia bidii darasani.

“Mahangaiko yalinipa jukwaa la kutambua kwamba katika kila hali ngumu unayopitia, unapaswa kujifunza kitu kipya ma kutokata tamaa ya maisha,” anasema.

Mchango kitaaluma

Salyne amekuwa mwalimu kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Amefunza katika shule nyingi za upili zikiwamo St Columban’s (Kitale), St Paul’s Mitiro (Bondo) na St Antony’s Boys (Kitale) kabla ya kuhamishiwa Immaculate Girls Mukuyu.

Anajivunia kuwakuza wanafunzi wengi katika sanaa ya utunzi wa mashairi, uigizaji na uandishi wa kazi bunilizi. Baadhi ya wanafunzi wake anaowajivunia na kuwaonea fahari kutokana na mapenzi yao ya dhati kwa Kiswahili ni mwalimu Simon Ekiru ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Cha Moi na mwigizaji maarufu David Kangogo almaarufu ‘David The Student’.

Kwa hakika, Salyne amefundisha na kufinyanga idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili. Si madaktari, si wanahabari, si walimu, si marubani, si wahandisi.

Upevu wa tajriba yake katika utahini wa Kiswahili ni kati ya mambo ambayo yamemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuinua kiwango cha lugha hii kwa kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu ibuka na mwafaka zaidi katika kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Immaculate Girls ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotangazwa.

Uandishi

Salyne ni mwandishi stadi ambaye amechangia pakubwa makuzi ya taaluma mbalimbali za Kiswahili.

Miongoni mwa vitabu ambavyo ameandika ni ‘Tamrini ya Ushairi’ (kimehaririwa na John Makete), ‘Kiswahili Tekelezi’, ‘Maarifa kwa Shule za Upili’, ‘Maswali na Majibu ya Kigogo’, ‘Fasiri ya Kidagaa Kimemwozea’ na ‘Mwongozo wa Kigogo’.

Kutokana na upana wa uzoefu wake kitaaluma, Serikali ya Kaunti ya Trans-Nzoia imempokeza mkataba wa kuwa msimamizi wa huduma zote za kutafsiri nyaraka na stakabadhi muhimu za kaunti.

Kwa sasa anashirikiana na wenzake Maria Mvati, James Kanuri na Saul Simon kuandaa vitabu vingine vya kiada kwa hisani ya Shirika la Huduma za Kielimu kwa Taifa (NES).

Tuzo

Salyne amewahi kutawazwa Mwalimu Bora wa Mwaka (TOYA) nchini Kenya mnamo 2015.

Alitambuliwa na kutuzwa pakubwa kwa mara nyingine mnamo 2018 kutokana na ufanisi wa wanafunzi wake wa Shule ya Upili ya Immaculate Girls waliowasilisha shairi la Kifaransa ambalo lilitia fora na kuibuka bora zaidi nchini kati ya mashairi yote mengine yaliyoshirikishwa katika mashindano ya kitaifa kwa ajili ya tamasha za muziki na drama.

Mwaka huu, wanafunzi wake walifana tena katika tamasha za kitaifa za muziki ambapo waliambulia nafasi ya tatu katika ngazi ya kitaifa iliyojumuisha zaidi ya washiriki arobaini kutoka kote nchini.

Changamoto

Salyne amekabiliana na misukosuko na mapito ya kila sampuli. Anasema yapo matatizo mengine yanayosababishwa na mikondo ya fikra zetu, mitazamo ya watu kutuhusu pamoja na ukosefu wa kuelewa jinsi ya kukabiliana na hali tofauti katika ulimwengu unaotuzunguka.

Kwa wakati fulani, nusura ajiuzulu baada ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu katika shule moja aliyokuwa akifundisha kuwanyima wanafunzi na walimu idhini ya kuzungumza Kiswahili shuleni.

“Ilikuwa hatia kuwasiliana kwa Kiswahili katika mazingira ya kazi. Tulihitajika kukitema Kiingereza pekee. Jambo hilo lilinikoroga nyongo, nikatamani kuachana kabisa na ualimu,” anasema.

You can share this post!

Van Persie afurahia kiwango cha kiungo Dani Ceballos

KINA CHA FIKIRA: Japo safari bado ndefu, ni hatua nzuri kwa...

adminleo