• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
WASIA: Mazoezi ya kimwili yana umuhimu katika maisha ya mwanafunzi

WASIA: Mazoezi ya kimwili yana umuhimu katika maisha ya mwanafunzi

Na HENRY MOKUA

BINADAMU ni mzembe kwa kawaida.

Hupenda kukamilisha kazi impasayo muda mfupi kabla ya wakati ufaao.

Ukimpa muda mwingi au mchache, atakawia tu kuimaliza kwa kujiambia: bado muda upo na hatimaye hulazimika kufanya kazi hiyo chini ya shinikizo kubwa hivi kwamba hata anaweza kujinyima usingizi.

Mwanafunzi ni binadamu hata zaidi katika muktadha huu. Yaani, yeye kwa kuwa hana wengi wa kumtegemea walivyo wazazi, huzembea hata zaidi.

Wakati mwingine, kutaja tarehe ya tukio mapema huwaziwa kuwa suluhu kwa uvivu huu.

Mathalani, ratiba za mitihani kitaifa ya mwaka huu ya shule za msingi na upili zilitolewa mapema tu, katika muhula wa kwanza.

Wakati huo lakini, wanafunzi wanaohusika waliiona mitihani hiyo ikiwa mbali sana. Sasa ndiyo kwanza wengi wao wanasoma usiku na mchana wasije wakajiaibisha. Lakini lipo swali la kimsingi na muhimu la kujiuliza – je, shinikizo hili laweza kuwa na athari gani?

Mojawapo ya masuala muhimu wanayoyapuuza vijana wakati huu ni mazoezi ya mwili. Husahau kwamba mazoezi haya yanafaa kuongezeka sawa na kazi ya kiakili. Kwa hivyo, hutumia muda mwingi kusoma bila kufanya mazoezi na kwa namna hii kukosa kuyadumisha wanayoyasoma katika kumbukumbu zao kutokana na akili kuchoka kupindukia. Ili kuepuka hasara itokanayo na kutofanya mazoezi ya mwili, mwanafunzi anapaswa kutenga muda kuyashiriki mara kwa mara. Zingatia manufaa yafuatayo ya mazoezi ya mwili.

Mazoezi huathiri seli za ubongo moja kwa moja kwa kuimarisha afya ya seli zenyewe, wingi na uhai wazo. Je ni faida gani nyingine mwanafunzi ataitaka kuliko hii? Kando na athari hii chanya, mazoezi ya mwili huimarisha hali ya akili, kufanikisha usingizi kwa muda ufaao, kupunguza msongo na wahka – mambo ambayo yakikosekana husababisha matokeo duni ya kiakademia.

Kwa hivyo hatua ya kuchukua ni gani? Anza kufanya mazoezi. Waweza kufanya mazoezi ya kutembea, kucheza mpira, kukimbia kidogo na mengineyo yatakayokufaa kulingana na mazingira yako.

Mazoezi ya nusu saa hivi kwa siku yatakuwa ya manufaa makubwa.

Kama huwezi kuanza na dakika 30 mara moja, waweza kuanza na robo saa hivi kisha ukaziongeza hatua kwa hatua. Ikiwa kutembea kunakoafadhalishwa zaidi hakuwezekani kwako, wazia kuogelea, kupanda vidato au kucheza densi.

Aidha, kazi za nyumba kama kupiga deki kwa dakika kadhaa au zoezi jingine linaloweza kuufanya moyo wako kupiga kwa kasi laweza kufaa.

Ukiona huna nidhamu ya kuhakikisha unashiriki mazoezi haya mwenyewe, jiunge na rafiki anayefanya mazoezi mara kwa mara au kumwomba rafiki mwenyewe kukutathmini.

Rafiki huyu anaweza kuhakikisha umeyashiriki na kuangalia unavyoendelea ili kukupa hamasa ya kuendelea zaidi hadi ufikiapo azimio lako.

Jitolee kuyafanya mazoezi kawaida kwako au tukio la mara kwa mara kwako sawa na kutumia dawa inayokupasa ili kupona maradhi fulani. Tangu hapo, wajuao husema kuwa mazoezi ni dawa au matibabu na hivyo kuwa msingi wa kuthaminiwa sana na yeyote atakaye kufanikiwa, hasa mwanafunzi.

Usije ukangoja kesho, anza leo. Tenga muda na kufanya mazoezi machache leo.

Zidisha kwa akali fulani kesho na kesho kutwa. Ukiendelea hivi utaona kazi yako ya kusoma na kudurusu ikianza kuwa nyepesi na kukuweka katika nafasi nzuri ya kutimiza ndoto zako za kiakademia iwapo utajumuisha mazoezi haya na kusoma kiasi kinachostahiki. Kila la heri!

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Japo safari bado ndefu, ni hatua nzuri kwa...

NDIVYO SIVYO: Ufaafu wa ngoja, ngojea, ibwa na ibiwa katika...

adminleo