• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
NDIVYO SIVYO: Ufaafu wa ngoja, ngojea, ibwa na ibiwa katika miktadha anuwai

NDIVYO SIVYO: Ufaafu wa ngoja, ngojea, ibwa na ibiwa katika miktadha anuwai

Na ENOCK NYARIKI

KUNA makosa mawili ambayo hufanywa na watu wanapokusudia kuwaambia wenzao kusubiri.

Baadhi yao husema “ongoja” ilhali wengine husema “ngojea”.

Kauli ya kwanza si mwafaka kwa sababu ‘‘ongoja’’ si neno la Kiswahili. Kauli ya pili ni faafu kwa kiasi fulani kutegemea muktadha wa matumizi.

Tutatoa maelezo zaidi kuhusu madai haya ila tuseme kwamba kauli za kutendea, kutendwa na kutendewa za neno iba pia huibua utata katika mazungumzo.

Baadhi ya watu husema “wameniiba” wakiwa na maana ya “wamenipokonya.’’ Kauli hii mbayo yamkini hutokana na athari ya lugha za kwanza za watu huibua maana tofauti kabisa na ile ambayo hudhamiriwa.

Tamko “wameniiba” linaweza kuchukuliwa kumaanisha “wamenichukua mimi”.

Aidha, kauli “Pesa zangu zimeibiwa” japo imezoeleka sana katika mawasiliano huenda isiwe na maana ya “pesa zangu zimechukuliwa na mtu fulani bila idhini yangu”.

Mnyambuliko katika kauli ya kutendea huwa na maana mbalimbali. Kwanza, humaanisha kitendo fulani kimetendwa kwa niaba ya mtu mwingine, mtu huyo akanufaika kwa mema au kwa mabaya.

Pili, kwamba kitendo kimetendewa mahali fulani. Mfano: Walimshikia mwizi shuleni. Maana nyingine za kauli hii hujitokeza vyema katika miktadha tofauti. Mathalani, tunaposema: Juma anamwonea sana, kauli hii ina maana ya “anamfanyia yasiyo haki”.

Hata hivyo, viambishi {e} na {i} ambavyo hutumiwa kunyambulia maneno katika kauli hii vinaweza pia kuibua dhana ya kutenda. Jambo hilo hufanyika hivyo kwa nadra ili kutofautisha maana. Hii ndiyo sababu iliyotufanya kusema kuwa kauli ‘‘wameniiba’’ haiwezi kuwa na maana sawa na ‘‘wameniibia’’.

Minyambuliko katika kauli za kutendwa na kutendewa hutagusana mno katika baadhi ya miktadha hivi kwamba haiwi rahisi kung’amua dhana iko katika kauli gani mpaka ijitokeze katika sentensi.

Mfano mzuri ni maneno tobolewa, ngojewa, pokelewa na bomolewa ambayo yanaweza tu kueleweka katika muktadha wa sentensi.

Kimsingi, kauli ya kutendewa huibua dhana kuwa mtu fulani amefanyiwa kitendo ili aweze kuathirika kwa mema au mabaya.

Mtu huyu hahitaji kufanya chochote kuhusiana na kitendo hiki.

Maneno mengine yanaweza kupambanuliwa vyema kwa kutumia kauli ya kutendwa na kutendewa. Kwa mfano, dhana “ibwa” imo katika kauli ya kutendwa ilhali “ibiwa” imo katika kauli ya kutendewa. Kwa hiyo, mtu anaposema “pesa zangu zimeibwa” kauli hii huibia fasili kuwa “mtu fulani amechukua pesa zangu.”

Dhana ngoja nayo ina maana ya subiri ilhali ngojea inaweza kuwa na maana ya kusubiri ukiwa mahali fulani au kusubiri kwa niaba ya mtu mwingine.

You can share this post!

WASIA: Mazoezi ya kimwili yana umuhimu katika maisha ya...

SEKTA YA ELIMU: TVET vyaweza kufaulishwa kwa rasilimali...

adminleo