SENSA: Wakenya wahakikishiwa usalama wao
Na SAMMY WAWERU
SHIRIKA la Takwimu Nchini (KNBS) limehakikishia taifa kuwa katika sensa itakayofanyika usiku wa Agosti 24 na 25, mikakati kabambe imewekwa ili kuimarisha usalama.
Meneja wa KNBS Vivianne Nyarunda amesema Alhamisi kwamba uteuzi wa maafisa watakaoendesha shughuli hiyo ulizingatia maeneo wanayoishi.
“Tulipowateua, tulizingatia wanatoka katika vijiji watakavyohudumu. Tunahakikishia wananchi kwamba ni vijana mnaowajua,” akasema Bi Nyarunda.
Zaidi ya watu 165,000 waliteuliwa kuendesha shughuli hiyo.
Visa vya mafunzo ya maafisa kuvurugwa vimeripotiwa katika baadhi ya maeneo, wakazi wakilalamikia ubaguzi katika uteuzi.
Kando na kuandamana na maafisa wa polisi, Nyarunda amesema watatembea na wazee wa mitaa na machifu, hivyo basi usalama utaimarishwa ipasavyo.
Baadhi ya wananchi wanakosoa hatua ya kuendesha shughuli hiyo usiku kwa sababu za kiusalama.
Hata hivyo, Vivianne amesema Wakenya wengi mchana huwa kazini, ikizingatiwa kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alisisitiza Jumatano kuwa siku zilizotengewa sensa 2019 hazitatangazwa likizo ya kitaifa.
Waziri aliagiza Jumatano na leo Alhamisi kwamba baa na vituo vyote vya burudani nchini kufungwa saa kumi na moja jioni wikendi hii ili sensa ifanyike usiku kucha baina ya Agosti 24 na 25.
Tofauti kati ya Huduma Namba na sensa
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru amesaidia kutegua kitendawili baada ya kuangazia maswali ambayo yamekuwa yakiibuliwa ni kwa nini serikali ifanye sensa ilhali data zilizokusanywa wakati wa usajili wa Huduma Namba zinaweza kutumika kutambua takwimu au idadi ya wananchi.
Shughuli za usajili wa Huduma Namba zilifanyika kati ya Aprili 25 hadi Mei 29, 2019, ikikadiriwa walipa ushuru waligharamia kima cha kati ya Sh5-6 bilioni.
Sensa, shughuli ya kitaifa kuhesabu watu, hufanyika kila baada ya miaka 10, na mwaka 2019 imeratibiwa kufanyika Agosti 24 na 25.
Mucheru amesema data za Huduma Namba haziwezi kutumika kutambua takwimu za wananchi Kenya.
Kulingana na Bw Mucheru ni kwamba shughuli za Huduma Namba zilipania kusajili na kutambua raia walioko nchini, ambapo mbali na kushirikisha Wakenya, pia raia wa kigeni walisajiliwa.
“Data za sensa zinahusisha Wakenya pekee, na tunahitaji kujua mengi zaidi. Kwa mfano, tuna wakulima wangapi nchini? Takwimu na data tutakazopata zitawezesha serikali kupanga mikakati yake ya ugavi wa raslimali na maendeleo kwa kipindi cha miaka 10 ijayo,” akasema Mucheru akihutubu katika kikao na waandishi wa habari, Harambee House jijini Nairobi.
Waziri huyo alikuwa ameandamana na mawaziri Ukur Yattani (Fedha) na Dkt Fred Matiang’i ambapo walieleza kuhusu maandalizi ya sensa 2019.
Kwa upande wake waziri Yattani amesema serikali imejiandaa kwa shughuli hiyo ya kitaifa pamoja na mikakati kabambe kuwekwa kuifanikisha.
Pia, amefafanua mfumo wa teknolojia utakaotumika kukusanya data na idadi ya maafisa wa muda walioteuliwa.
Dkt Matiang’i amehakikishia taifa kuwa usalama wakati wa sensa utaimarishwa kikamilifu.
Shughuli hiyo ya mnamo Jumamosi, Agosti 24 na Jumapili 25, itafanyika kati ya saa kumi na mbili za jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.
“Watakaoendesha shughuli hiyo wataandamana na maafisa wa usalama na machifu, watakaokuwa na sare rasmi pamoja na wazee wa kijiji,” akasema waziri Matiang’i, akiongeza kwamba waliodhinishwa na KNBS ndio wataruhusiwa kufanya sensa.
Dkt Matiang’i pia aliagiza maafisa wote wa polisi walio likizoni kurejea kazini mara moja.
KNBS inasema watakaokuwa safarini watahesabiwa katika vituo vya magari watakavyokuwa.
Sensa hufanyika kila baada ya miaka 10, na kulingana na serikali shughuli hii itasaidia katika upangaji wa mgao wa raslimali na utekelezaji wa maendeleo.
Aidha, sensa 2019 inapaniwa kugharimu takriban Sh18.5 bilioni.