• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
KEROCHE: KRA yajitetea baada ya kuelekezewa mishale na watumiaji mitandao ya kijamii

KEROCHE: KRA yajitetea baada ya kuelekezewa mishale na watumiaji mitandao ya kijamii

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) imetoa taarifa Alhamisi kutetea hatua ya kukamatwa kwa wamiliki wa kampuni ya kutengeneza pombe na mvinyo ya Keroche Breweries Limited, Afisa Mkuu Mtendaji Bi Tabitha Karanja na mumewe ambaye pia ni mwenyekiti Bw Joseph Karanja.

Hii ni baada ya baadhi ya Wakenya kutuma jumbe mitandaoni wakiishutumu KRA kwa kile wamedai ni kuhujumu biashara zilizoanzishwa na wajasiriamali humu nchini.

Wafanyabiashara hao, wamekamatwa Alhamisi asubuhi kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru unaofikia kiasi cha Sh14.5 bilioni.

“Madai haya hayana msingi wowote kwani tumekuwa tukilipa ushuru na ada zote zinazohitajika kwa mujibu wa sheria. Hizi ni njama za kufifisha biashara zilizoanzishwa na Wakenya, na ambazo zimechangia ukuaji wa uchumi,” akasema Bi Karanja mnamo Jumatano jioni dakika chacha baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuamuru wakamatwe.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Keroche Breweries Limited, Tabitha Karanja aelekezwa na wapelelezi mara baada ya kumkamata Agosti 22, 2019, mjini Naivasha kuhusiana na tuhuma za kukwepa ushuru wa zaidi ya Sh14 bilioni. Picha/ Macharia Mwangi

Lakini katika taarifa yake saa chache baada ya kukamatwa kwa wamiliki hao wa Keroche Breweries, KRA imesema hivi:

“Wakenya hawafai kuhadaiwa kuwa KRA inapiga vita watu fulani au biashara za Wakenya. Badala yake, ni muhimu ifahamike kuwa KRA ina wajibu wa kufanikisha biashara chini ya mazingira faafu ya kuziwezesha kunawiri. Na hiyo itawezekana tu ikiwa zitalipa ushuru kulingana na sheria,” ikasema.

Vilevile, KRA imetoa wito kwa wafanyabiashara na watu binafsi ambao hawajakuwa wakizingatia sheria kwa kulipa ushuru kujiwasilisha na kuzilipa.

“Tunawahimiza kushirikiana na afisi za KRA na kituo vya huduma kote nchini kufanya malipo hayo. KRA imejitola kuwaongoza katika mchakato wa kukadiria na kulipa ada hizo kwa manufaa ya taifa lao,” mamlaka hiyo ikasema kwenye taarifa hiyo iliyotumwa kwa mashirika ya habari.

KRA imefafanua kuwa itaendelea kuwakabiliwa wale ambao hukwepa ushuru kimakusudi kwa njia mbali mbali kama vile kufeli kufichua kiwango cha mapato yao.

Wengine pia hukwepa ushuru kwa kuandaa taarifa za kupotosha kuhusu gharama zao za uzalishaji, kufeli kulipa ushuru wa kuingiza bidhaa nchini kwa kuficha bidhaa, utathmini batili wa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje, miongoni mwa njia zingine za ukora.

Awali, viongozi kadhaa pia walijitokeza kutetea wamiliki hao wa Keroche Breweries wakisema “wananyanyaswa bila sababu.”

Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui ameitetea kampuni hiyo akisema huchangia pakubwa ukuaji wa uchumi wa nchini kwa kutoa nafasi za ajira.

“Tunakosoa njia hii ambayo KRA inatumia kuhakikisha kuwa kampuni za humu nchini zimetii sheria ya ulipaji ushuru. Wawekezaji wa asili ya Kenya hawafai kudhulumiwa jinsi hii kana kwamba wao ni wahalifu ilhali wanachangia uimarishaji wa uchumi wa nchi,” akasema Bw Kinyanjui kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Naye kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen ameishauri KRA kusaka njia mbadala za kushughulikia visa vya ukwepaji ushuru badala ya “kuwaaibisha wawekezaji wa humu nchini kiasi hiki.”

“Nakubali kwamba ukwepaji ushuru ni uhalifu na ikizingatiwa kuwa kuna uhaba wa ajira nchini, naomba KRA ijadiliane na wanaoshukiwa kukwepa kulipa ushuru badala ya kuwavamia kama wezi wa kimabavu,” akasema Bw Murkomen, ambaye ni Seneta wa Elgeyo Marakwet, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi pia ameitaka serikali kuwaandama wakwepaji ushuru lakini sio kwa “njia za kikatili kama inavyowafanyia wafanyabiashara Humprey Kariuki na Bw na Bi Karanja.”

  • Tags

You can share this post!

Ukumbusho wa umma wa kifo cha Mzee Kenyatta wafikia kikomo

UFUGAJI KIBIASHARA: Amepiga hatua kuu maishani kwa ufugaji...

adminleo