• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Wamiliki wa Keroche watiwa nguvuni

Wamiliki wa Keroche watiwa nguvuni

Na MACHARIA MWANGI na BENSON MATHEKA

WAMILIKI wa kampuni ya kutengeneza pombe na mvivyo ya Keroche mjini Naivasha, Tabitha Karanja na mumewe Joseph Karanja, walikamatwa Alhamisi kwa madai ya kutolipa ushuru wa zaidi ya Sh14 bilioni.

Mnamo Jumatano, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji, aliagiza wawili hao wakamatwe.

Bi Karanja alisema kwamba alilazimika kukesha katika ofisi yake Jumatano akiogopa kukamatwa na maafisa wa polisi waliopiga kambi nje ya kampuni yake, muda mfupi baada ya Bw Haji kuagiza watiwe nguvuni.

Maafisa hao wa polisi walishika doria katika kampuni hiyo kwa magari zaidi ya manne hadi mwendo wa saa nne jana asubuhi wakurugenzi hao waliposalimu amri na kujipeana mikononi mwao.

Akiongea na Taifa Leo kwa simu kabla ya kukamatwa, Bi Karanja, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, alisema alishangazwa na amri ya kumkamata.

Mfanyabiashara huyo alidai kwamba alifahamu amri hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

“Sijawahi kuitwa na idara yoyote kuhusu suala hilo na ninashangaa na kushtushwa na hali hii,” akasema.

Bw Haji aliagiza wawili hao wakamatwe na kufunguliwa mashtaka 10 ya kukwepa kulipa ushuru, makosa anayodai walifanya kati ya Januari 2015 na Juni 2019.

Ombi la kutokamatwa

Walikamatwa mjini Naivasha, muda mfupi baada ya wakili wao Irungu Kang’ata kuwasilisha ombi katika Mahakama Kuu jijini Nairobi kuzuia polisi kuwakamata.

Hata hivyo, ombi hilo halikuweza kusikilizwa kwa sababu majaji wako Mombasa kwa kongamano lao la kila mwaka na ilibidi faili itumwe huko.

Kwenye taarifa aliyotoa Jumatano usiku, Bi Karanja alimlaumu Bw Haji kwa kutoa agizo la kumkamata ilhali kuna kesi kortini kuhusu suala hilo.

Alhamisi, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen walikosoa hatua ya Bw Haji wakisema kuna njia mbadala za kushughulikia masuala ya kukosa au kuchelewa kulipa ushuru.

Kukamatwa kwa Bi Karanja na mumewe kulifanyika siku chache baada ya mfanyibiashara mwingine, Humprey Kariuki kufuguliwa mashtaka ya kukosa kulipa ushuru wa mabilioni ya pesa.

You can share this post!

Nisingekuwa sogora bila Messi – Ronaldo

Maraga ahimiza Wakenya kuwafichua maafisa fisadi

adminleo