• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Korti yaidhinisha mwanamke aliyepatikana na hatia ya kuua mtoto wa mke mwenza atalikiwe

Korti yaidhinisha mwanamke aliyepatikana na hatia ya kuua mtoto wa mke mwenza atalikiwe

Na KATE WANDERI na MARY WANGARI

MWANAMKE aliyehukumiwa kifo mnamo 2004 kwa kumuua mtoto wa mke mwenzake miaka 20 iliyopita atajutia milele baada ya korti kuvunjilia mbali ndoa yake, baada ya mumewe kuwasilisha kesi ya talaka.

Hakimu Mkuu Nakuru Elizabeth Usui, mnamo Ijumaa, Agosti 23, amevunjilia mbali ndoa kati ya Bw James Waithaka na mkewe Ann Wangari, kuhusiana na kitendo chake cha kinyama kilichosababisha mauaji ya mwana wa mumewe ambapo wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16.

Ikifutilia mbali ndoa hiyo, korti imeeleza kwamba kitendo cha Wangari kilikuwa kimemsababishia mumewe uchungu mwingi na mateso kisaikolojia, hali iliyoruhusu uamuzi huo wa talaka.

“Mlalamishi amewasilisha msingi mzuri unaounga mkono kesi yake katika kutoa uamuzi wa kufutilia mbali ndoa yake. Amri ya kuvunjilia mbali ndoa hiyo sasa imetolewa,” amesema hakimu.

Uamuzi huo unajiri baada ya Bw James Waithaka kuwasilisha kesi akitaka kumtaliki mkewe, Wangari, akisema kwamba ndoa yao haingedumu tena na suluhisho la pekee lilikuwa kuivunja.

Wangari amekuwa akitumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya korti kumpata na hatia ya kumuua mtoto wake wa kambo, Dunstan Wambugu.

Aidha, korti ilieleza kwamba, licha ya Wangari kupelekewa mashtaka na kutia sahihi nakala katika Gereza la Wanawake la Langata, alikosa kujibu mashtaka na kuilazimu mahakama kutoa uamuzi kuhusu suala hilo bila upande wa kujitetea.

“Nimepata kwamba malalamishi hayajapingwa na ushahidi wa mlalamishi haujakanushwa. Nimeridhishwa na ushahidi wa mlalamishi kuhusu kuvunjilia mbali uhusiano huo,” amesema hakimu.

Awali akitoa uamuzi wake, Jaji Alnashir Visram alishawishika kwamba, Wangari alikuwa kweli amemuua kijana huyo chipukizi kwa sababu alikuwa na mgogoro na watoto wanne wa mke mwenzake aliowachukia kupindukia.

Walioana mnamo 1993 katika ndoa ya kitamaduni ambapo walipatiwa cheti cha ndoa na kujaliwa watoto wawili.

Alipinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu lakini rufaa yake ilitupiliwa mbali mnamo 2007, baada ya majaji wa Mahakama ya Rufaa kukubaliana na uamuzi huo.

Bw Waithaka aliondoka kortini akiwa ameridhika baada ya ndoa, aliyoieleza kama ambayo haingeokolewa, kuvunjwa.

“Ndoa iliyorasimishwa kati ya wahusika hawa wawili basi imefutiliwa mbali kwa misingi ya ukatili kutoka kwa mshtakiwa,” korti iliamua.

Wangari aliyekuwa mke wa pili wa Bw Waithaka, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani mnamo 2004.

You can share this post!

Wakuu wa Keroche waachiliwa kwa dhamana

Kitabu chenye mada zinazohusu ICC na changamoto ya uhalifu...

adminleo