Habari Mseto

Wandayi amfurusha katibu 'aliyeshindwa' kujibu maswali

August 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KATIBU wa Wizara ya Ustawishaji wa Kiviwanda Betty Maina alifurushwa Alhamisi kutoka kikao cha kamati moja ya bunge la kitaifa baada ya wabunge kumsuta kwa kutokuwa makini kwa kazi yake.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, Bi Maina alitakiwa kujibu maswali yaliyoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya fedha katika idara.

Wabunge wanachama wa kamati hiyo walitaka kujua kwa nini wizara yake haikuwasilisha stakabadhi husika wakati wa ukaguzi wa matumizi ya fedha katika mwaka wa kifedha wa 2016/2017.

“Mbona wizara yako iliwasilisha stakabadhi hitajika miezi kadha baada ya wakaguzi kukamilisha kazi yao?” akauliza Bw Wandayi.

Lakini Katibu huyo, ambaye alionekana kuchanganyikiwa, alisema kuwa hajui ni kwa nini maafisa wa wizara yake walifeli kuwasilisha stakabadhi hizo kwa wakati kwa wakaguzi.

Ajitetea

Bi Maina alisema hakuwa na habari hizo kwa sababu hakuwa Katibu wa Wizara wakati ukaguzi huo uliendeshwa.

Hata hivyo, nakala za stakabadhi – hasa taarifa ya kifedha – zilizowasilishwa mbele ya kamati hiyo ya PAC zina sahihi yake.

“Ikiwa stakabadhi zilikuwepo na hazikuwasilishwa, je, stakabadhi hizo ni sahihi au huenda zilivurugwa kwanza kabla ya kuwasilishwa ili kuficha ukweli kuhusu hitilafu au sakata fulani?” akauliza Mbunge wa Tongaren Dkt Eseli Simiyu.

Baada ya mabishano yaliyodumu robo saa, wabunge walikataa kukubali maelezo ya Bi Maina na wakamkashifu kwa kujaribu kukwepa maswali yao.

Hapo ndipo mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Wandayi alipositisha kikao hicho ili kumpa Katibu huyo muda wa kuandaa majibu ipasavyo.

“Katika hali hii, haitakuwa sawa kwetu kuendelea na majadiliano hayo. Nenda ujiandae vizuri kujibu maswali ya kamati hii,” Bw Wandayi akaamuru.

Kulingana na ripoti hiyo ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, wizara hiyo haingeelezea asili ya madeni yake ya kiasi cha Sh115,863, 748.

Bw Ouko pia aliibua maswali kuhusu namna wizara hiyo ilitumia jumla ya Sh157,972,498 katika ununuzi wa mashine maalum, vifaa na mitambo mbalimbali.

Hii ni kwa sababu vocha za malipo hazikuwasilishwa kwa maafisa wa ukaguzi kama inavyohitajika kisheria.