Habari

Rasharasha na kijibaridi kikali katika maeneo mengi kipindi cha sensa

August 24th, 2019 2 min read

Na CAROLYNE AGOSA

RASHARASHA za mvua na baridi kali ni hali ya hewa inayotarajiwa katika kaunti zaidi ya 30 wakati shughuli ya kuhesabu watu, Sensa, ikitarajiwa kung’oa nanga leo Jumamosi jioni.

Wakazi na maafisa wa Sensa katika maeneo ya Ziwa Victoria, Magharibi nyanda za juu za Bonde la Ufa na kanda ya Pwani watashuhudia vipindi vya jua asubuhi vitakavyofuatiwa na mvua za radi saa za alasiri.

Kulingana na utabiri wa hali ya hewa wa siku tano zijazo, kuanzia leo Ijumaa hadi Jumanne mvua inatarajiwa kunyesha katika kaunti za Kisumu, Siaya, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia.

“Vipimo vya juu vya joto katika kaunti hizo vitafikia nyuzijoto 30 katika vipimo vya sentigredi huku vya chini vikishuka hadi nyuzijoto 10,” ilisema taarifa ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa.

Maeneo machache ya Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale yatashuhudia rasharasha za mvua asubuhi na alasiri. Vipimo vya juu zaidi vya joto vitagonga nyuzi 30 huku vya chini vikifika nyuzi 21.

Kaunti za Turkana, West Pokot na Samburu pia zitakuwa na mvua za radi maeneo machache huku viwango vya joto maeneo mengi vikiwa kati ya nyuzi 24-35.

“Baridi na mawingu yanatarajiwa katika kaunti za Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka nyakati za asubuhi vikiandamana na vipindi vya jua. Saa za alasiri kutakuwa na rasharasha za mvua katika maeneo mengi,” ilieleza taarifa hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara Stella Aura.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa eneo pana la mashariki mwa nchi litashuhudia vipindi vya jua kwa wingi vikiandamana na upepo mkali, unaotazamiwa kupepea hadi ukanda wa Pwani na kusababisha mawimbi makali katika Bahari Hindi.

Wakazi wa kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado na Taita Taveta watashuhudia jua kuwaka kwa wingi mchana wote wa siku hii ya Sensa.

Viwango vya joto katika kaunti hizo vitabadilika pakubwa; vya chini zaidi vikifika nyuzi kati ya 08-15 huku joto la juu zaidi likigonga nyuzi kati ya 27-36.

Shughuli ya kuhesabu watu kote nchini itaanza leo saa kumi na moja jioni na kuendelea kwa siku saba hadi Agosti 31.

Siku zitakazotiliwa mkazo zaidi ni leo Jumamosi 24 na Jumapili 25. Wakenya wote watatakiwa kuwa nyumbani kuanzia saa kumi na moja jioni na Jumapili ili wahesabiwe.

Maafisa wa serikali wakiongozwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i wameagiza kwamba hakutakuwa na kesha ama sherehe za kibinafsi usiku, baa zitafungwa saa kumi na moja jioni, na watu hawataruhusiwa kutembea usiku Jumamosi na Jumapili ili kufanikisha hesabu ya watu wengi zaidi katika siku hizi mbili.