• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Shughuli zatatizika Knut kutokana na ukosefu wa fedha

Shughuli zatatizika Knut kutokana na ukosefu wa fedha

Na OUMA WANZALA na MARY WANGARI

SHUGHULI za Chama cha Kitaifa cha Walimu nchini (Knut) zimetatizika baada ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kukosa kukata ada za muungano kutoka kwa mishahara ya walimu na kuziwasilisha kwa wadau.

Tatizo hilo la kifedha ambalo limetokana na mgogoro kati ya Knut na TSC sasa limesababisha zaidi ya matawi 110 kote nchini kupunguza shughuli zake huku yakisubiri suala hilo kutatuliwa.

Haya yamejiri huku Katibu Mkuu Wilson Sossion akisema hakuwa akipigana na serikali bali alitaka kuhakikisha maslahi ya walimu anaowawakilisha yanazingatiwa na akaitaka TSC kutoa hela.

Maafisa kadha katika matawi walisema hali ni mbaya mno kiasi kwamba wafanyakazi kama vile makatibu, wasaidizi ofisini, na walinzi hawajalipwa kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Mikutano ya matawi ya kila mwaka pia imesitishwa kutokana na changamoto hiyo. Maafisa hao pia walisema taasisi za kifedha zinawaandama kuhusiana na mikopo ambayo haijalipwa.

Knut hupokea Sh140 milioni kila mwezi kutoka kwa TSC kama ada za muungano.

Bw Sossion alikiri kuwa muungano huo unakabiliwa na matatizo ya kifedha kutokana na ukosefu wa hela.

“Tunaisihi TSC itoe fedha ili tuweze kuendesha shughuli zetu ipasavyo,” alisema Sossion.

Mahakama

Wiki iliyopita, Jaji wa Mahakama kuhusu Mahusiano ya Leba, Bi Maureen Onyango aliamrisha TSC kutoa ada za muungano kutoka kwa wanachama wa Knut za Sh140 milioni.

Alitoa uamuzi huo baada ya Knut kufika kortini kulalamikia uamuzi wa TSC wa kupunguza mishahara ya walimu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Mnamo Januari mwaka huu, TSC iliagizwa kupatia Knut ada ya uwakala lakini ikakataa na kupatia kundi hasimu la Muungano wa Walimu wa Shule za Msingi (Kuppet).

Knut inadai imenyimwa Sh50 milioni kila mwezi kutoka kwa maelfu ya walimu wasio wanachama. Kuppet imekuwa ikipokea hela hizo kutoka kwa walimu kwa asilimia 1.8 ya mshahara.

Fedha hizo hutozwa walimu wasio wanachama wanaonufaika kutokana na manufaa yanayopiganiwa na muungano.

Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Muungano Mkuu wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU, Francis Atwoli aliwahimiza maafisa wa muungano huo kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na kuepuka malumbano yasiyo na maana..

“COTU (K) inasisitiza kuwa tofauti zinazodhihirishwa katika uongozi wa Knut hazihusu maslahi ya walimu wanapohudumu na tunatahadharisha uongozi wote wa Knut dhidi ya kuhadaiwa na siasa za utengano kutoka nje zinazolenga kuvunja muungano na kusababisha migawanyiko miongoni mwa walimu kwa sababu hali hii itadhoofisha muungano,” ilisema taarifa ya Atwoli.

  • Tags

You can share this post!

Kongamano lajadili maswala muhimu ya kuinua wanawake

DAU LA MAISHA: Nesi wa kwanza nchini kushughulikia saratani

adminleo