• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
UMBEA: Kuna mawimbi katika ndoa, upende usipende, yatatokea

UMBEA: Kuna mawimbi katika ndoa, upende usipende, yatatokea

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA ndoa huwa ni ndoano kwa baadhi ya wanandoa.

Kwamba katika maisha yao ya kuwa pamoja imekuwa ni kupanda milima mfululizo, kiasi kwamba wanalemewa na kuishiwa na pumzi na hali ikizidi wengine huamua kujitoa kwenye hiyo barabara.

Ndoa sio lelemama. Na wale wenye roho nyepesi, si ajabu kuwaona wakitoroka nyumba zao, mwezi mmoja tu baada ya kuolewa.

Unapooa ama kuolewa, kuna mawimbi na misukosuko ambayo upende usipende itatokea. Kuna wanaume watakaokuabisha. Wakawa na macho juu na kutongoza kila apitaye mbele yake.

Kuna wale visirani, ambao kila kukicha anatafuta sababu ya kuanzisha zogo. Lakini pia wapo wale wazuri, ndio, hata wazuri pia wapo.

Katika wote, wale ambao huleta sokomoko ndani ya nyumba ni wale wanaotongoza na kutembea na wasichana wa kazi ndani ya nyumba.

Mwanaume wa aina hii, atamvizia mkewe akisafiri, akienda shughuli zake ama hata wakati mwingine akiwepo nyumbani na kuvinjari na ‘anti’ ambaye jukumu lake ni kusaidia kazi za nyumbani.

Kwa wale akina dada ambao busara zao zimeishia puani, huamua kulipiza kisasi na wao kuanza uhusiano wa kujazia pengo lililotengenezwa na mume. Ukifanya hivi dada, utakuwa unajikaanga kwa mafuta yako mwenyewe.

Mtu wa kwanza kumshughulikia ni mumeo na sio mwanamke mwingine ama hata msichana wa kazi. Usipigane na mwanamke mwenzako sababu ya mwanaume.

Muhimu, usiache nyumba yako, sababu ya mwanaume. Iwapo hakuna kipigo na anatimiza mahitaji ya familia, kuondoka nyumbani kwako sababu ya mwanamke mwingine, sio suluhisho la shida zako. Pambana na hali yako hadi kieleweke.

Ndoano nyingine inawahusu akina kaka wanaoishi kwenye ndoa bila kufurahia matunda ya ndoa. Hawa ni wale wanaonyimwa tunda la roho na wake zao na kuendeshwa mfano wa magari mabovu. Kwamba inapita mwezi mmoja, mume amenyimwa unyumba. Bwana atabembeleza wee… lakini bibi anakuwa mgumu kuliko jiwe akidhani anamkomoa mume wake.

Matokeo yake yanakuwa nini? Bwana anaamua kujituliza mawazo baa, akitoka kazini anashika chupa hadi saa saba ama nane usiku.

Akirudi nyumbani ni hoi bin taaban, anajitupa kitandani na nguo na viatu. Simlaumu hata kidogo mwanaume anayefanya hivi, afanye nini kingine?

Na wanawake wengine ni majuha, mume akirudi asubuhi, naye kesho anaenda kupiga mitungi hadi asubuhi anarudi nyumbani yuko chakari.

Anapofungua mlango, anakaribishwa na mizigo yake inamngoja nje ya nyumba yake.

Wanadada wengine hupatwa na ndoano ya kumeza chakula bila kutafuna, kwamba miaka nenda hawajawahi kufurahia burudani na waume zao.

Kutoridhika

Kwa mwanaume kusema mimi mwenzio sijatosheka, ni jambo la kawaida, lakini kwa mwanamke huona kama mwenziwe atamfikiria vibaya labda ana tabia za ukahaba.

Unajikuta unaacha njiani lakini kwa woga wako na kuona si haki kusema sijatosheka, niongeze dozi, unameza chakula bila kutafuna wala kuhisi ladha yake

Matokeo yake unalalamika pembeni kuwa mpenzi wako hakuridhishi wakati ulikuwa na uwezo wa kumweleza ukweli kuwa “mimi mwenzio bado, kwani ndio kwanza asubuhi kunakucha.

Kama unaona aibu kuzungumza na mwenzio, basi tumia matendo.

Tumia vitendo vyenye ladha murua ili kumpa taarifa ya hisia zako.

Siku zote matatizo ya mapenzi humalizwa na wapenzi wenyewe na wala usijidanganye eti mpenzi wako asipokuridhisha utoke nje, huo sio ufumbuzi wa matatizo yako.

Iwapo unakasirishwa mume anaporudi asubuhi, fikiria pia mumeo atajihisi vipi unaporudi asubuhi ama unapoamua kumnyima haki yake ya unyumba.

 

[email protected]

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Mahaba bila pato ni kama hadithi ya...

Cheruiyot apeperusha bendera Kenya ikipata matokeo mseto...

adminleo