Habari

Sensa yaja na mzaha wa kila aina katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii

August 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

PICHA ya mwanamume mmoja aliyebeba chupa kadhaa za bia tayari kuzipakia kwenye gari, ambayo imekuwa ikisambaa mitandaoni ni kielelezo cha jinsi ambavyo baadhi ya watumiaji majukwaa hayo wameingiza mzaha katika amri zilizotolewa na serikali kuhusu shughuli ya kuhesabu watu inayoanza Jumamosi saa kumi na mbili jioni.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i aliamuru kwamba baa zote na vilabu vya burudani – kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa kumi na mbili alfajiri – kufungwa ili kutoa nafasi kwa makarani kuwapata watu nyumbani.

Sasa inavyoashiriwa kwenye picha ya mtu huyo aliyebeba bia, baadhi ya waraibu wa pombe huenda kweli wamejipanga na kununua pombe ya kutosha kwenda kunywa wakiwa nyumbani ili wasijipate katika mkono mbaya na serikali.

Maelezo kwenye picha hiyo yako katika lugha ya Kiingereza lakini fasiri yake ni: Matayarisho ya sensa yamenoga. Ikiwa hatutaenda kwa baa, basi tutaleta baa kwetu. Anavyoamini Waititu.

Hapa Waititu ametajwa. Huyu ni Gavana wa Kaunti ya Kiambu ambaye mahakama iliamua akae kando wakati ambapo anakabiliwa na kesi ya kutoa kandarasi kwa mkarabati wa barabara katika hali za kutatanisha.

Waititu amewahi kusema kwamba ni heri kuhamisha mikondo ya mito; hasa Nairobi River, badala ya kubomoa majengo ya kibiashara.

Nao mashabiki wa soka, hasa timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu nchini Uingereza Arsenal na Liverpool, wameikosoa amri ya Dkt Matiang’i.

Hii ni kwa sababu amri kwamba vilabu na kumbi za burudani zifungwe saa kumi na moja jioni itawanyima fursa ya kutizama mechi baina ya timu hizo mbili zitakazopambana kuanzia saa moja na nusu usiku (7.30 pm).

“Huwa inachosha sana kufuatilia mechi ukiwa nyumbani. Utanunua wapi kinywaji timu yako ikifunga bao?” akauliza shabiki mmoja anayetumia jina @mwangi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Mwingine alipeleka mzaha katika hatua nyingine akitoa chaguo au jinsi mbili.

“Matiangi kuna vitu viwili tu. Ama tunahesabiwa kwa baa au kwa seli. Lakini tutakuwa kwa baa kutazama mechi ya Arsenal na Liverpool,” akaandika.