Habari

Simhitaji Raila 2022 – Kalonzo

August 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CAROLYNE AGOSA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka, amesema hahitaji usaidizi wa kinara wa ODM, Raila Odinga, ili kushinda kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Badala yake, Bw Musyoka alisema tayari ameanza kujitafutia uungwaji mkono wa Wakenya akijitayarisha vilivyo kwa kivumbi cha 2022, pasipo kumtegemea Bw Odinga kufaulu katika kinyang’anyiro hicho.

Bw Musyoka alisema aliweka kando azma yake ya kuwania urais mara mbili ili kumuunga mkono Bw Odinga, na kwamba sasa ni wakati wake kutwaa uongozi.

“Huwezi kuomba uongozi, uongozi hunyakuliwa,” alikariri makamu huyo wa Rais wa zamani.

Alikuwa akizungumza Ijumaa katika ibada ya mazishi ya babake Mwakilishi wa Wanawake Joyce Kamene, Mzee David Kasimbi.

Viongozi kadha wa eneo la Ukambani, ambako ndiko ngome ya Bw Musyoka, wanataka makamu huyo wa Rais wa zamani kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu 2022.

Waliendelea kumshinikiza Bw Musyoka kuwa mstari wa mbele katika muungano wowote wa kisiasa utakaoundwa kuelekea uchaguzi mkuu 2022.

Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama aliwashauri wanasiasa wanaosaka kura za Ukambani kuzungumza na Bw Musyoka kwanza.

Bw Muthama alisema: “Mkitaka kuongea na sisi ongeeni na Kalonzo kama mmoja wa vigogo wakuu wa kisiasa humu nchini.”

Mbunge wa Mavoko, Patrick Makau alisema kuwa Bw Musyoka anatosha kuwa Rais!

“Mwaka 2022 itakuwa kuchagua kati ya nani fisadi na si fisadi. Katikati yetu tuko na mwanamume mweupe kama pamba; anaitwa Stephen Kalonzo Musyoka,” aliambia waombolezaji.

Ni kauli iliyoungwa mkono na mbunge wa Mwala Vincent Musyoka aliyeongeza kuwa “Raila Amolo Odinga anafaa kukupatia nafasi sasa!”

Matamshi hayo yaliashiria kuendelea kutawanyika kwa vigogo wa muungano wa NASA waliojumuisha Bw Musyoka, Bw Odinga, Musalia Mudavadi wa ANC na Seneta Moses Wetang’ula wa Ford Kenya.

‘Mwamba ngoma…’

Vinara wa NASA katika siku za hivi karibuni wamejitokeza kujipigia debe, kila mmoja akivutia ngoma upande wake.

Muungano huo uliojumuisha vyama tanzu vya ODM, Wiper, ANC na Ford Kenya katika uchaguzi mkuu uliopita 2017, uliwakilishwa na Bw Odinga.

Hata hivyo, mambo yamebadilika tangu wakati huo huku Bw Odinga akiingia katika mkataba wa amani, almaarufu handisheki, na Rais Uhuru Kenyatta.

Ni hatua iliyowafanya wenzake kuhisi wametengwa huku Seneta wa Bungoma Bw Wetangula akijiondoa na chama chake cha Ford Kenya kwenye muungano.

Bw Musyoka ni kinara wa pili aliyesalia katika zizi la NASA kutangaza wazi wazi kwamba atawania urais 2022 kivyake.

Bw Mudavadi ndiye alijitokeza mbeleni wa kwanza kutangaza msimamo wake kwamba atakuwa kwenye debe.

Bw Odinga anapigiwa upato na wengi kutangaza kuwania kwake urais 2022, lakini amekuwa akipuuzilia mbali minong’ono hiyo.