• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Kenya Simbas, Zimbabwe wasajili ushindi raga ya Victoria Cup

Kenya Simbas, Zimbabwe wasajili ushindi raga ya Victoria Cup

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa raga ya wachezaji 15 kila upande ya Victoria Cup mwaka 2010 Kenya Simbas na mwaka 2011 Zimbabwe wamezoa ushindi muhimu Jumamosi.

Simba ya kocha Paul Odera imerarua Zambia 31-16 uwanjani RFUEA jijini Nairobi kupitia penalti tatu na mkwaju kutoka kwa Isaac Njoroge nao nahodha Curtis Lilako, nahodha msaidizi Elkeans Musonye, Toby Francombe na Brian Amaitsa wakachangia mguso mmoja kila mmoja.

Kenya ilienda mapumzikoni kifua mbele 18-13 baada ya Zambia kufunga mguso, penalti na mkwaju.

Ikiwa na ufahamu mkubwa ilipoteza dhidi ya Zambia mara ya kwanza zilikutana uwanjani humu 23-9 mwaka 1976, Simbas ilirejea dakika 40 mnyama tofauti.

Pia, ilinufaika na Zambia kucheza dakika 24 za mwisho watu 14 baada ya mchezaji wake kuonyeshwa kadi nyekundu. Zambia ilipachika alama zake kupitia kwa Laston Mukosa (penalti mbili, mguso na mkwaju), Edward Mumba (mguso).

Kenya, ambayo ilichabanga Zambia 23-10 mwaka 1980 na 33-10 mwaka 2004 uwanjani RFUEA, sasa itahitaji kulipiza kisasi dhidi ya Zimbabwe katika mechi ya marudiano uwanjani humu itakapoalika mabingwa hao watetezi mnamo Septemba 21 ili kurejesha taji ililopoteza.

Zimbabwe ilichabanga Kenya 30-29 zilipokutana wiki chache zilizopita mjini Bulawayo.

Ushindi huu ni wa kwanza wa kocha Odera tangu achukue usukani mwezi Mei 2019.

Alianza enzi yake kwa kulemewa 16-13 na Uganda katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Elgon Cup kabla ya kukosa ushindi wa Simbas wa 16-5 dhidi ya Uganda katika mechi ya marudiano jijini Kampala akiwa nchini Brazil kwa raga ya dunia ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 na pia ilipopiga Zambia 43-23 mjini Kitwe.

Kichapo

Alikaribishwa kwenye benchi la kiufundi kutoka mapumziko ya raga ya dunia kwa kichapo dhidi ya Zimbabwe, ambayo imedumisha rekodi yake ya kutoshindwa katika kampeni za mwaka huu kwa kubwaga Uganda 32-26 jijini Harare, Jumamosi.

Zimbabwe inasalia juu ya jedwali baada ya kupiga Zambia jijini Harare (29-10), Kenya mjini Bulawayo (30-29) na Uganda jijini Kampala (31-26). Kenya ni ya pili baada ya kulima Uganda 16-5 jijini Kampala na Zambia 43-23 mjini Kitwe katika mechi zake zingine.

Nambari tatu ni Uganda, ambayo imeshinda mechi moja. Ilipepeta Zambia 38-22 jijini Kampala. Zambia inavuta mkia katika mashindano haya ya mataifa manne bila alama.

  • Tags

You can share this post!

Sensa yaanza kote nchini maafisa wakiambiwa kulinda vifaa

SENSA MWAKA 2019: Naibu Rais, viongozi kadhaa tayari...

adminleo