• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
‘Inabidi Wanyama ajisuke upya kumridhisha Pochettino’

‘Inabidi Wanyama ajisuke upya kumridhisha Pochettino’

Na GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur sio shirika la kutoa misaada kwa wachezaji, bali wachapakazi.

Huo ndio ujumbe wa Mauricio Pochettino kwa kiungo Mkenya Victor Wanyama, ambaye mchango wake Spurs ulipungua zaidi katika msimu miwili iliyopita kiasi cha kocha huyo kutoka Argentina kumuona kama mzigo.

Vyombo vya habari nchini Uingereza viliwahi kumnukuu Pochettino akimtaja Wanyama kama “mnyama” kutokana mchango wake mkubwa uliomfanya kuwa tegemeo.

Hata hivyo, Pochettino, ambaye aliwahi kuwa mkufunzi wa Wanyama katika klabu ya Southampton kabla ya kumleta Spurs, hakumeza maneno yake Ijumaa alipoulizwa kuhusu hali ya Wanyama katika klabu ya Spurs kabla ya mechi dhidi ya Newcastle United itakayosakatwa Jumapili.

Alionya, “Hapa ni kazi tu. Soka ni leo na kesho, sio jana. Unahitaji kila mara kuonyesha unastahili kuwa hapa.”

“Kuhusu Wanyama, alipata jeraha na mchezaji mwingine akaimarisha mchezo wake na kujaza nafasi yake kikamilifu. Hii ni timu ya soka, si shirika linalosaidia wachezaji wanaohitaji msaada. Nasema wazi kuwa jibu hili halihusu Wanyama pekee kwa sababu ukweli ni kuwa sisi si shirika la kusaidia wachezaji wasiojiweza uwanjani. Hapa ni mchango wako uwanjani utakuokoa na benchi la kiufundi lina wachezaji wengi wa kuchezesha katika nafasi tofauti. Mimi ndiye kocha, nahitaji kufanya uamuzi huo na natumai utajitokeza kuwa wa busara. Victor ni mchezaji muhimu sana na kwa sababu tofauti, alipiga hatua nyuma katika mchezo wake. Mambo huwa hivyo katika soka. Kwa kawaida vitu kama hivi hutokea katika klabu zote,” alisema kocha huyo pengine akiashiria kuwa nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya ameshapiga kutu.

Wanyama, ambaye alihusishwa na uhamisho hadi klabu za Bournemouth, West Ham, Brighton, Southampton, Sheffield United kabla ya kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uingereza kifungwe Agosti 9, pia alihusishwa na Galatasaray nchini Uturuki, Celtic (Scotland) na sasa Club Brugge (Ubelgiji) na AS Monaco (Ufaransa).

Hata hivyo, ripoti zimekuwa zikisema anakaribia kujiunga na Club Brugge, ambayo inasemekana ilimfanyia uchunguzi wa kimatibabu Agosti 22. Klabu za Spurs na Brugge zinasemekana vimekubaliana bei na kilichosalia ni Wanyama kuafikiana na Brugge kuhusu mshahara. Analipwa Sh8.0 milioni kila wiki.

You can share this post!

Umuhimu wa mkulima kumiliki kipimio chake

SOKA MASHINANI: Mang’u Stars FC

adminleo